Hizbullah yajibu mapigo, yashambulia vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi kadhaa za Israel kaskazini mwa maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu mwaka 1948, kama sehemu ya awamu nyingine ya operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya utawala huo na kuwatetea watu wa Gaza.
Taarifa iliyotolewa na Hizbullah imesema kwamba, imelenga vitongoji vya walowezi vya Shlomi na Goren ikijibu mashambulizi yaliyofanywa na Israel dhidi ya raia, hasa mashambulizi ya utawala huo katili katika miji ya Naqoura na Tayr Harfa ambayo yameua takriban wahudumu tisa wa Hizbullah na harakati ya Amal.
Wapiganaji wa Hizbullah pia Alhamisi iliyopita walishambulia kituo cha kamandi ya jeshi la Israel kilichoundwa hivi karibuni huko Liman, katika eneo la Magharibi mwa Galilaya, kuwaunga mkono watu wa Gaza.
Hizbullah pia imetoa mkanda wa video uliowarekodi wapiganaji wake wakilenga mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel huko Horsh Ramim karibu na mpaka wa kusini wa Lebanon na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Harakati hiyo pia imerusha maroketi kadhaa katika mji wa Kiryat Shmona, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Utawala haramu wa Israel umekuwa ukishambulia maeneo ya kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana ulipoanzisha mashambulizi makubwa huko Gaza na kuua Wapalestina wasiopungua 32,552, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.