Ripoti: Magaidi walioua watu 143 Moscow walipokea maagizo kutoka Ukraine
Ripoti ya wachunguzi wa Russia imethibitisha kuwepo ushahidi kwamba magaidi walioshambulia ukimbi wa Crocus jijini Moscow walipokea fedha kwa siri kutoka Ukraine, nchi muitifaki wa Marekani ambayo iko vitani na Russia.
Hayo yamedokezwa na Kirill Kabanov, mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Rushwa ya Russia ambaye amesema katika mahojiano na Sputnik kwamba data katika vifaa vya kiufundi vilivyonaswa kutoka kwa washukiwa wa shambulio hilo la kigaidi imethibitisha uhusiano wa magaidi hao na Ukraine.
Takwimu za awali zilizopokelewa kutoka kwa waliokamatwa katika kesi inayohusiana na shambulio hilo la kigaidi zilionyesha Ukraine ilihusika pakubwa katika shambulio hilo.
Kabanov amebainisha kuwa ripoti mpya ya Kamati ya Uchunguzi ya Russia inabainisha kuwa mashirika ya kijasusi ya Ukrine yamehusika katika kuratibu hujuma hiyo ya kigaidi na kuwa ni muhimu kufahamu kuwa mashirika hayo ya kijasusi ya Ukraine yana uhusiano wa moja kwa moja na shirika kuu la kijasusi la Marekani, CIA na mashirika ya kijasusi ya Uingereza ya MI6 na MI5.
Kabanov, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Russia, ameongeza kuwa, “ndiyo maana nchi za Magharibi zinajaribu kuficha ukweli huku zikidai kuwa kundi la kimataifa la kigaidi lililopigwa marufuku ndilo lililohusika ili kuficha ukweli kwamba Ukraine yenyewe ni shirika kubwa la kigaidi."
Hujuma ya kigaidi ya Machi 22 katika ukumbi wa tamasha wa Crocus City Hall katika mji wa Krasnogorsk, nje kidogo ya Moscow ilipelekea kuuawa watu wasiopungua 143. Washukiwa wakuu wanne katika hujuma hiyo - wote raia wa Tajikistan – wameshakamatwa nchini Russia na wameshtakiwa kwa ugaidi.