Viongozi wa harakati za Palaestina za Hamas na Jihad Islami wakutana Tehran
Ismail Haniyah, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amekutana mjini Tehran na Katibu Mkuu wa Harakati ya Palestina ya Jihad Islami Ziyad al-Nakhaleh.
Hamas ilisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba mkutano huo ulilenga kujadili matukio ya kisiasa na ya medani kuhusiana na vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.
Wajumbe wa pande zote mbili wamesifu harakati za muqawama na watu wa Gaza katika kukabiliana na uvamizi wa Israel.
Taarifa hiyo imesema: "Aidha, viongozi hao wawili wamejadili juhudi za kukomesha vita, na kusisitiza kwamba mafanikio ya mazungumzo yoyote yasiyo ya moja kwa moja yanategemea mambo manne ya kimsingi: kusimamishwa kabisa vita, kuondoka kikamilifu wanajeshi vamizi wa Isarel katika ukanda wote wa Gaza; kurudi kwa watu waliokimbia makazi yao, kuingia misaada na mahitaji ya msingi kwa watu wa gaza, pamoja na kubadilishana wafungwa."
Taarifa hiyo imebainisha kuwa: "Harakati hizo mbili pia zimelaani vitendo vya utawala vamizi wa Isarel katika mji wa Al-Quds (Jerusalem) na Msikiti uliobarikiwa wa Al-Aqsa, yakiwemo mashambulio na ukiukaji wa sheria, sambamba na uvamizi na mauaji katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan."
Viongozi wa harakati zote mbili katika taarifa yao pia "wamepongeza operesheni za harakati za muqawama huko Yemen, Iraq na kusini mwa Lebanon, ambazo zinathibitisha umoja wa makundi ya muqawama na kwamba watu wa Palestina hawako peke yao katika kukabiliana na uvamizi huu na wale wanaoshirikiana nao."
Hali kadhalika viongozi wa Hamas na Jihad Islami wametoa shukrani zao kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake wa kimkakati kwa wapiganaji wa Kiislamu au wanamuqawama na wananchi wa Palestina na misimamo yake thabiti katika kuunga mkono haki zao za kitaifa.
Harakati hizo mbili zimelaani "mauaji ya kila siku ya uvamizi na uchokozi wa kinyama unaofanywa na utawala haramu wa Isarel dhidi ya Wapalestina, na kuahidi kuzidisha juhudi za mshikamano, haswa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani."
Viongozi hao wa Hamas na Jihad Islami wiki hii wamekutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa Tehran katika nyakati tofauti.