Israel na Hamas: Nini kimetokea kwa Hamas baada ya miezi sita ya vita Gaza?

 

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kabla ya tarehe 7 Oktoba Hamas ilikadiriwa kuwa na wapiganaji wapatao 30,000.

Miezi sita imepita tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel kufanyika kwa mara ya kwanza tarehe 7 Oktoba,2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.

Katika kukabiliana na shambulio hili, Israel iliahidi "kuliangamiza na kulimaliza kundi la Hamas" ili lisiwe tishio tena, na kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi huko Gaza ambayo imesababisha vifo vya watu zaidi ya 33,000, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya kundi hili.

Israel inasema imewaua maelfu ya wapiganaji wa Hamas na kuharibu sehemu kubwa ya mahandaki ambayo wanamgambo wa Kipalestina waliyajenga chini ya Gaza na kutumika kutekeleza mashambulizi yao.

Lakini je, Israel imefanikisha lengo lake la kuliangamiza kundi hilo la wanamgambo? Na Wapalestina sasa wanafikiria nini kuhusu viongozi wao na viongozi wa Hamas huko Gaza baada ya vita vya umwagaji damu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo lao?

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Zaidi ya asilimia 70 ya watu waliouawa Gaza ni wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya.

Je, Israel ilifanikiwa kuwaondoa viongozi wa Hamas?

Timu ya BBC Verify ilichunguza taarifa na machapisho ya mitandao ya kijamii kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) na kugundua kuwa, kwa mujibu wa ripoti zilizonukuu makamanda wa IDF, kabla ya Oktoba 7, iliaminika kuwa Hamas ilikuwa na wapiganaji 30,000 huko Gaza.

Viongozi wengi wa kisiasa wa Hamas, kama vile Ismail Haniyeh, anayechukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa kisiasa wa kundi hilo, wanaishi nje ya nchi.

Haniyeh anaishi Qatar, mbali na vita na Israeli. Hata hivyo, Jumatano wiki iliyopita, yeye mwenyewe aliripoti kuwa watoto wake watatu na wajukuu wake kadhaa waliuawa katika shambulio la anga la IDF.

Jeshi la Israeli lilidai kuwa ndugu hao watatu walikuwa "wanachama wa kijeshi wa Hamas" na kuthibitisha kuwa "wamewaangamizi".

Sehemu kubwa ya muundo wa uongozi wa kijeshi wa Hamas unaaminika kuwa ndani ya Gaza.

Katika taarifa ya hivi punde , jeshi la Israel limesema limewaua takriban wapiganaji 13,000 kutoka kundi hili la Palestina tangu kuanza kwa vita, bila ya kutaja ni kwa namna gani limehesabu idadi hiyo.

Hamas kwa upande wake ilitangaza kuwa imepoteza wapiganaji 6,000.

Israel pia inachapisha majina ya viongozi wa Hamas ambao inasema wamekufa, lakini haiwezekani kuthibitisha kama kweli ni wanachama wa kundi hilo.

Kwa mfano, Mustafa Thuraya, ambaye alifanya kazi kama mwandishi wa habari wa kujitegemea kusini mwa Gaza, alikuwa katika kitengo hiki wakati gari lake lililengwa na shambulizi la Israeli mnamo Januari. BBC pia ilipata nakala ya orodha hiyo.

Tangu mwezi Oktoba, Israel imerekodi vifo 113 vinavyoaminika kuwa wanachama wa Hamas, wengi wao wakiwa wamekufa katika miezi mitatu ya kwanza ya vita.

Na mwaka huu, iliripoti kifo cha Marwan Issa, naibu kamanda wa tawi la kijeshi la Hamas, alikuwa nambari 3 katika kundi na alikuwa mmoja wa watu wanaotafutwa sana nchini Israel.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Viongozi wa juu wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, akiwemo Yahya Sinwar, wanaaminika kuwa bado wako hai.

Nje ya Gaza, Israel ilishutumiwa mwezi Januari kwa kuhusika na mlipuko uliomuua kiongozi wa kisiasa wa Hamas Saleh al-Arouri katika kitongoji cha Dahiyeh, kusini mwa Beirut, Lebanon.

Hata hivyo, wataalamu waliohojiwa na BBC walisema viongozi wengi wa kundi hilo huko Gaza wanaaminika kuwa bado yuko hai.

"IDF ilishindwa kuwafikia viongozi waandamizi wa Hamas," anasema Mairav Zonszein, mchambuzi wa masuala ya Israel na Palestina katika kundi la kimataifa la utatuzi wa migogoro.

Je, jeshi la Israel lilifanikiwa kuharibu mtandao wa mahandaki la Hamas mjini Gaza?

f

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Hamas imesema mahandaki yake yana urefu wa kilomita 500, ingawa hii haiwezi kuthibitishwa.

Kama sehemu ya ahadi yake ya kulitokomeza kundi la Hamas, Israel ilisema kuwa itaharibu mtandao mkubwa wa mahandaki ambayo kundi hilo la wanamgambo limejenga chini ya Gaza na kutumia kusafirisha silaha, bidhaa na watu.

Hamas imesema mtandao wake wa mahandaki unaenea kilomita 500, ingawa hakuna njia ya kuthibitisha hilo.

BBC ililiuliza jeshi la Israel ni kiasi gani cha mtandao wa handaki waliharibu. Walijibu kwamba vikosi vyao "vimeharibu miundombinu mingi ya kigaidi huko Gaza."

Kwa hakika, bado kiongozi wa kundi hilo - na mwenye nguvu - ni Yahya Sinwar, Mohammed Deif na viongozi wengine kadhaa waliohusika na shambulio hilo la Oktoba 7.

Katika jaribio la kubaini kiwango cha mtandao wa jumla wa mahandaki yaliyogunduliwa na vikosi vya Israeli, BBC ilichunguza machapisho ya IDF kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii ya Telegram ikimaanisha mahandaki ya Gaza, kati ya terehe 7, 2023 na tarehe 26 Machi, 2024.

Ujumbe mwingi hautoi maelezo sahihi au maeneo maalum, kwa hivyo haiwezekani kuthibitisha ni mahandaki mangapi na ni uwiano gani ndani ya mtandao uliogunduliwa au kuharibiwa na IDF.

Kati ya jumbe 36 zilizopitiwa na BBC, zilielezea kuwa kuna jumla ya mashimo ya 400 za handaki yalibainika . Hata hivyo, kusema hiyo ndio idadi kamili itakuwa ni kupotosha, anasema Dr Daphné Richemond-Barak, mtaalam wa vita vya chini ya ardhi na profesa katika Chuo Kikuu cha Reichman nchini Israeli.

Uharibifu rahisi wa mashimo ya mahandaki huacha mtandao wa mahandaki uliendelea kuwa sawa, anaamini mtaalam. Anaongeza: "Sidhani kama tumeona uharibifu wa jumla wa mahandaki wakati wa vita hivi.

Kwa hivyo, uchambuzi uliowasilishwa mwezi Machi na ujasusi wa Marekani unatabiri kwamba kushindwa kwa Israel katika jaribio lake la kumaliza mtandao mkubwa wa Hamas wa mahandaki yatasababisha kundi hilo kuendelea na upinzani wake kwa miaka mingi.

"Israel huenda ikakabiliwa na upinzani wa silaha kutoka kwa Hamas katika miaka ijayo, na jeshi litakuwa na ugumu wa kuondoa miundombinu ya chini ya ardhi ya Hamas, ambayo inaruhusu waasi kujificha, kurejesha nguvu na kuvishangaza vikosi vya Israeli," ripoti hiyo ya mpelelezi wa ujasusi , Avril Haines ilisema.

Miezi sita baada ya vita, Wapalestina wanafikiria nini kuhusu viongozi wao katika Ukingo wa Magharibi na Gaza?

"Ulipizaji kisasi mkubwa" ulioahidiwa dhidi ya Hamas na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu haujawa tu na athari kwa Gaza.

Katika maeneo mengine ya Palestina, Ukingo wa Magharibi, Israel imefanya mashambulizi kadhaa ya kikatili dhidi ya makundi yenye silaha wakati ambapo raia wasio na hatia wameuawa. Pia imewakamata maelfu ya watu ambao bado wanazuiliwa bila kufunguliwa mashtaka.

Wakulima wa Kipalestina wamefukuzwa kutoka katika ardhi yao kufuatia vurugu ambazo wakati mwingine husababisha vifo, na pia kampeni ya vitisho na walowezi wa Kiyahudi wenye msimamo mkali.

Hata hivyo, kura za maoni zinaonyesha uungaji mkono mkubwa miongoni mwa Wapalestina kwa mashambulizi yaliyofanywa na Hamas mnamo Oktoba 7.

Profesa wa sayansi ya siasa na mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kisiasa na Uchaguzi cha Palestina (PCPSR) ,Khalil Shikaki, aliiambia BBC kwamba hata wale ambao hawapendelei Hamas wanakubali jinsi mashambulizi dhidi ya Israeli yamefanikiwa katika kutekeleza mapambano ya uhuru wa Palestina hadi mwisho.

PCPSR ni shirika huru la utafiti wa kura za maoni lenye makao yake mjini Ramallah, mji mkuu wa Ukingo wa Magharibi, ambalo limekuwa likichunguza na kutathmini maoni ya umma katika maeneo ya Palestina kila robo tangu mwaka 1990.

Katika kura ya maoni ya hivi karibuni ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Gaza mwezi Machi, asilimia 71 ya waliohojiwa walisema waliidhinisha uamuzi wa Hamas kuanzisha mashambulizi yake mwezi Oktoba.

Pia waliulizwa ni nani walidhani ataibuka mshindi kutoka kwa vita hivi, Hamas au Israel, na asilimia 64 walisema Hamas.

Kuhusu suala la kuwaunga mkono viongozi wao, maoni ya washiriki yanaendelea kuonyesha uungaji mkono mkubwa wa Hamas, ambayo imetawala Gaza tangu mwaka 2007, na kumkataa Mahmoud Abbas, rais wa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina, ambayo inasimamia Ukingo wa Magharibi na ambayo inaungwa mkono. ya Magharibi.

Kura hiyo ya maoni ilionyesha kuwa asilimia 70 ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi waliridhishwa na utendaji wa Hamas katika vita, wakati asilimia 14 tu walimuunga mkono Abbas.

Kura ya maoni ya hivi karibuni ya Wapalestina ilionyesha kukataliwa kwa kiasi kikubwa kwa Mahmoud Abbas, ambaye anatawala Ukingo wa Magharibi na anaungwa mkono na nchi za Magharibi.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kura ya maoni ya hivi punde ya Wapalestina ilionyesha kumkataa kwa kiasi kikubwa Mahmoud Abbas, ambaye anatawala Ukingo wa Magharibi na kuungwa mkono na nchi za Magharibi.

Walipoulizwa ni nani watampigia kura iwapo kutakuwa na uchaguzi wa urais na wagombea wawili – Mahmoud Abbas wa Fatah na Ismail Haniyeh wa Hamas - asilimia 37 walisema wangemchagua Haniyeh na asilimia 11 tu ndio wangemchagua Abbas.

Katika Ukingo wa Magharibi, Mahmoud Abbas anaonekana kutokuwa na umaarufu. Kura ya maoni ilionyesha kuwa asilimia 93 ya watu wa West Bank wanataka rais wao ajiuzulu. Katika Ukanda wa Gaza, asilimia 71 walisema Abbas anapaswa kujiuzulu.

Je, Hamas itakuwa na mustakabali wa kisiasa Gaza baada ya vita?

Unaweza pia kusoma

Wengi wameuliza swali la nani atatawala Gaza baada ya vita, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyeweza kujibu hilo.

Kwa upande wa Israel, tunachojua ni maoni yaliyowasilishwa mwezi Februari na Benjamin Netanyahu, ambayo hayakujumuisha Mamlaka ya Palestina katika serikali ya baadaye ya Gaza.

Mpango wa waziri mkuu, kwamba Israel itadumisha udhibiti wake wa kijeshi juu ya eneo hilo kwa muda usiojulikana, umekosolewa vikali na wachambuzi kote ulimwenguni.

Kama mwandishi wa BBC wa idhaa ya Kiarabu Ethar Shalaby anavyoeleza, matukio mbalimbali yamewasilishwa juu ya nani anaweza kutawala Gaza baada ya vita, yote kwa kuzingatia dhana zinazohusiana na ikiwa Netanyahu atabaki madarakani au nani atashinda uchaguzi wa rais katika majimbo.

"Baadhi ya matukio yaliyowasilishwa ni pamoja na uwezekano wa kurejea kwa Mamlaka ya Palestina katika eneo la kisiasa huko Gaza, lakini maono mengine yanaiondoa," anasema Shalaby.

"Pia kuna uwezekano wa kuwepo kwa vikosi vya kijeshi vya kikanda katika awamu ya mpito, wakati kundi lingine linasubiri kuundwa kwa serikali ya kiraia chini ya udhibiti wa vikosi vya usalama vya Israeli.

"Lakini hakuna hata moja ya matukio haya yanayoweza kuthibitishwa, kutokana na uharibifu na mauaji ambayo yamefanyika hadi sasa Gaza," anaelezea mwandishi huyo.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Miezi sita baada ya kuanza kwa vita, sehemu kubwa ya Gaza ni magofu.

Pengine jambo pekee la uhakika ni kwamba maono yote hayahusishi jukumu la Hamas katika serikali yoyote ya baadaye ya Gaza.

Lakini wataalamu wanasema itakuwa vigumu sana Mamlaka ya Utawala wa Palestina mjini Gaza kutokuwa na au kuwa na uhusiano na Hamas kwa kiwango fulani.

"Haiwezekani kumuondoa kila mtu ambaye ana uhusiano wowote na Hamas," Sarah Yerkes, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya kimataifa ya masuala ya amani ya Carnegie, ameiambia BBC.

"Ninaelewa hamu ya kuiondoa Hamas madarakani na kuondoa uwezo wake wa kuidhibiti Gaza, lakini sidhani kama ni kweli kwa Waisraeli kutarajia kwamba yeyote ambaye alifanya kazi chini ya serikali inayoongozwa na Hamas anaweza kuondolewa madarakani.

"Hakutakuwa na urasimu kabisa na hakuna mtu mwenye uzoefu wa kutawala Gaza," mtaalamu huyo alisema.

Maafisa wa Hamas wanaripotiwa kushiriki katika mazungumzo ili kuruhusu mamlaka mpya ya Palestina kuchukua udhibiti wa Gaza kupitia serikali mpya ya watendaji wenye taaluma.

Profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar huko Gaza, Dr. Mukheimer Abu Saada, anaamini kuwa hili ni chaguo linalowezekana zaidi kwa Gaza baada ya vita.

"Hii ni hali inayowezekana kwa sababu ni jambo linalokubalika zaidi kwa Marekani na nchi za Kiarabu," mtaalamu huyo aliiambia BBC.

Na anaongeza kuwa : "Itakuwa serikali mpya, na mawaziri wapya ambao hawana uhusiano wowote na Hamas. " Nadhani serikali hii itapokelewa vizuri na Washington na jamii ya kimataifa, na hata kama Netanyahu hapendi, hana budi kukubali hilo."

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo