Kamanda Mwandamizi: Israel imeshindwa na Muqawama Ghaza, viongozi watamatishe vita
Yitzhak Barik, Jenerali mstaafu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa jeshi la utawala huo haramu limeshindwa na Muqawama wa Palestina katika vita vya Ukanda wa Ghaza na kutaka viongozi wa utawala huo watangaze utamatishaji wa vita hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Palestina SAMA,
Jenerali Barik amebainisha kuwa, malengo ya utawala haramu wa Israel
yaliyopelekea kuanzisha mashambulio dhidi ya Ghaza bado hayajafikiwa na
akasema, Israel inapaswa kutangaza uhitimishaji wa vita huko Ghaza.
Barik ameongeza kuwa, kuivamia kijeshi Rafah, mji wa kusini mwa
Ukanda wa Ghaza, hakutausaidia vyovyote utawala huo, kwa sababu Israel
imeshindwa katika vita na Muqawama.
Jenerali huyo mstaafu wa jeshi la utawala wa Israel unaofanya
mauaji ya kimbari ametamka bayana kuwa, hakuna nguvu inayoweza
kuuangamiza moja kwa moja Muqawama ili usiwepo tena.
Baada ya kupita zaidi ya miezi sita tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uivamie Ghaza bila ya kupata matunda wala mafanikio yoyote, utawala huo unazidi kuzama kwenye kinamasi cha migogoro yake ya ndani na nje siku baada ya siku.
Katika muda wote huu, utawala katili wa Kizayuni haujapata mafanikio mengine isipokuwa ya kufanya jinai, mauaji, uharibifu, uhalifu wa kivita, kukiuka sheria za kimataifa, kushambulia mashirika ya utoaji misaada na kulinakamisha kwa njaa eneo la Ghaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, tangu Oktoba 7, 2023
vilipoanza vita ya kinyama na mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa
Israel katika Ukanda wa Ghaza, hadi sasa watu elfu 34,049 wameuawa
shahidi na wengine elfu 76,901 wamejeruhiwa.../