Kwa mara ya kwanza, Hizbullah yashambulia ndani kabisa ya ngome za Wazayuni tangu vilipoanza vita vya Ghaza
Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo viwili vya kiejshi vya utawala wa Kizayuni wa Israel kulipiza kisasi cha mauaji ya wapiganaji wake wawili.
Shambulio hilo la jana la Hizbullah linaashiria operesheni ya kwanza kufanywa na Hizbullah ndani zaidi katika maeneo wanayokaa Wazayuni tangu vilipoanza vita vya Ghaza.
Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Hizbullah ya Lebanon imezishambulia ngome za kijeshi za utawala wa Kizayuni kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel kufuatia jinai za kinyama na za kutisha na umwagaji mkubwa damu za Wapalestina unaofanya utawala huo katika Ukanda wa Ghaza.
Mashambulio ya Hizbullah ambayo ni ya kuwaunga mkono wananchi wenye subira na uvumilivu mkubwa wa Ukanda wa Ghaza pamoja na Muqawama wa eneo hilo, yamezusha hofu kubwa kwa Wazayuni wanaoishi katika maeneo ya mpakani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hadi sasa makumi ya maelfu ya Wazayuni wamevihama vitongoji vya walowezi karibu na mipaka ya Lebanon kwa kuhofia mashambulizi ya Muqawama.../