Msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 26 wa Marekani kwa Israel sambamba na vita vya Gaza
Baada ya mabishano na mvutano kati ya Wademokrat na Warepublican na Hitilafu za pande hizo mbili juu ya msaada wa kigeni, Baraza la Wawakilishi la Marekani limeidhinisha kifurushi cha msaada wa dola bilioni 60 kwa Ukraine na kifurushi kiingine cha dola bilioni 26 kama msaada wa kijeshi kwa Israel kwa kura 366 dhidi ya 58.
Muswada huu lazima uidhinishwe na Seneti na kisha utiwe saini na rais wa Marekani ili kuwa sheria.
Kulingana na Wall Street Journal, huu ndio msaada mkubwa zaidi wa kijeshi kuwahi kutolewa na Marekani kwa Israeli tangu kuanza mashambulizi ya utawala huo haramu dhidi ya watu wa Ukanda wa gaza huko Palestina mnamo Oktoba 7 mwaka jana. Tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Israel imenufaika zaidi na msaada wa kijeshi wa Marekani kuliko nchi nyingine yoyote, na imekuwa ikiungwa mkono na vyama vya Republican na Democratic kwa muda mrefu.
Tangu baada ya kuanza mashambulio ya jeshi la Israel huko Gaza, serikali ya Biden imetangaza hadharani msaada wake wa kijeshi kwa Israeli mara mbili kwa uchache. Disemba mwaka jana, utawala wa Biden ulikubali kupeleka risasi 14,000 za vifaru na zana nyingine za kivita vyenye thamani ya zaidi ya dola milioni 253. Ikulu ya Rais wa Marekani, White House ilivuka kizuizi cha Kongresi kwa ajili ya kutuma msaada huo kwa kutumia Sheria ya Mamlaka ya Dharura ya Rais.
Pia, maafisa wa serikali ya Marekani wameripoti zaidi ya misaada mingine 100 ya kijeshi kwa Israel. Katika kipindi chote cha karibu miezi 7 ya vita vya Gaza, silaha zinazotengenezwa na Marekani zimekuwa zikitumiwa sana na jeshi la Israel huko Palestina. Ripoti zinaonyesha kuwa, silaha nyingi zinazotumika na Israel huko Gaza ni pamoja na mabomu ya kilo 450 au 900 kama vile bomu la Mark 84. Mwezi Machi maka huu, utawala wa Biden uliidhinisha kupelekwa mabomu 1,800 ambayo kila moja lilikuwa na uzito wa kilo 900, 500 na 225 aina ya Mark 84.
Katika miaka ya hivi karibuni, bajeti ya misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Israel imefafanuliwa katika mfumo wa kumbukumbu za miaka 10, na hati ya mwisho ilitiwa saini mnamo 2016, ambapo Washington iliahidi kutoa msaada wa kijeshi wa dola bilioni 38 kwa Israel kati ya miaka ya fedha ya 2019 na 2028.
Misaada mingi ya kijeshi ya Marekani kwa Israel inafafanuliwa kupitia programu ya "Ufadhili wa Kijeshi wa Kigeni", kwa Israel na hutumiwa kununua zana na huduma za kijeshi za Marekani.
Marekani pia huchangia takriban dola milioni 500 kila mwaka kwa mifumo ya pamoja ya ulinzi wa makombora.
Misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Israel pamoja na misaada yake ya kisiasa na kiuchumi daima imekuwa moja ya sababu kuu za kuchochea vita na kujitanua zaidi utawala huo na pia kuchangia sehemu kubwa katika kushindwa mazungumzo ya amani ya kuunda serikali mbili, na kuzidisha mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Sasa, na katika vita vya Gaza, Marekani imekuwa mshirika mkuu wa jinai za serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu, ambapo mikono ya nchi hiyo imejaa damu za watu wa Palestina.
Alaa kulli hal, misaada ya kijeshi na kiusalama ya dola bilioni 26 kwa Israel, katikati ya vita vya Gaza, inazidisha ushiriki wa Marekani katika uhalifu na jinai za utawala wa Kizayuni wa Isarel huko Palestina. Hii ni kwa sababu kwa kutoa misaada hii, serikali ya kivita na ya kifashisti ya Netanyahu itaendelea kukwepa mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.