Onyo jipya kuhusu kuingia NATO katika vita vya Ukraine


  • Onyo jipya kuhusu kuingia  NATO katika vita vya Ukraine

Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary amesema katika taarifa kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya Kijeshi ya Magharibi (NATO) wanauchukulia mzozo wa Moscow na Kyiv kuwa ni wao na wala hawazingatii hatari ya kujihusisha na mzozo huo. Ameonya kuwa NATO inakaribia kutuma askari wake huko Ukraine.

Katika mkesha wa uchaguzi wa Bunge la Ulaya, Orban amesema katika mkutano wa chama cha Fidesz cha Hungary kwamba: "Wanachama wengi huko Brussels wanaunga mkono vita, na siasa za Umoja wa Ulaya zimeratibiwa kwa mantiki hiyo." Orban pia amesisitiza kwamba Budapest haitaingia katika vita ikipendelea upande wowote, na kuonya kuwa Brussels inachezea moto kwa sababu vita kati ya Russia na Ukraine ni kinamasi ambacho kinaweza kuivuta Ulaya katika kina chake kirefu.

Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary

Onyo la Waziri Mkuu wa Hungary kuhusiana na uwezekano wa NATO kuingia katika vita vya Ukraine limetolewa kwa kuzingatia misimamo ya baadhi ya viongozi wa Ulaya, hasa Ufaransa, ya kuzihimiza nchi wanachama wa NATO ziingie katika vita vya Ukraine. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, baada ya kuwa mwenyeji wa mkutano uliohudhuriwa na viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi 20 mjini Paris, ameashiria kuwa hivi sasa hakuna maafikiano yaliyofikiwa kuhusu kutuma vikosi vya NATO kwenye uwanja wa vita. Pamoja na hayo ameweka wazi kuwa hakuna kitu kinachoweza kuzuia hilo kufanyika.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema katika kujibu matamshi ya Macron kuwa hakuna haja ya jeshi la Ufaransa kutumwa nchini humo madamu jeshi la nchi hiyo bado linapambana.

Bila shaka, kutumwa vikosi vya  NATO nchini Ukraine kutachukuliwa na Moscow kama  hatua ya kijeshi dhidi ya Russia na inaweza kukabiliwa na radiamali kali. Kwa murtadha huo, hatua hatari ya rais wa Ufaransa inaweza kuchochea chachu ya vita kati ya Russia na NATO na hatimaye vita vya tatu vya dunia.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Kwa kuzingatia suala hilo, msimamo wa Macron umekabiliwa na upinzani na ukosoaji wa wanachama wengi wa Umoja wa Ulaya, haswa Ujerumani, ambapo nchi hizo zimepinga kutumwa wanajeshi wa umoja huo huko Ukraine. Uingereza, Slovakia, Romania na Italia pia zimepinga suala la kutumwa vikosi vya jeshi la NATO Ukraine. Katika kujibu matamshi hayo ya Macron Boris Pistorius Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani amesema kutumwa wanajeshi wa Nato hakutasaidia kutatua matatizo ya Kyiv. Huku akitilia mkazo msimamo wake wa kutumwa askari jeshi wa Nato huko Ukraine, Rais wa Ufaransa amewataka waitifaki wa Kyiv wasiwe waoga kuhusiana na jambo hilo.

Jambo muhimu ni kwamba msimamo huo wa Macron umekakabiliwa na upinzani hata ndani ya Ufaransa yenyewe. Stephane Sejournay Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema: "Kwa sasa hakuna mpango wa kutuma vikosi vya kijeshi nchini Ukraine."

Kwa upande mmoja kufuatia kushindwa Ukraine katika mashambulizi yake dhidi ya jeshi la Russia katika majimbo ya mashariki na kusini mashariki mwa Ukraine, na kupungua misaada ya kijeshi na silaha ya Magharibi kwa upande mwingine, ni wazi kuwa suala hilo suala la  NATO kuingia  moja kwa moja katika vita hivyo kwa  kutuma askari wake katika mideni ya vita vya nchi hiyo dhidi ya Russia. Kufikia sasa, nchi za Magharibi zimekuwa zikitoa madai  ya kuisaidia kwa muda mrefu Ukraine, lakini  zimekuwa zikikanusha suala la kukabiliana moja kwa moja na vikosi vya Russia katika vita na Ukraine.

Kwa upande mwingine Rais Zelensky wa Ukraine, ambaye nafasi na satwa yake inaendelea kuporomoka siku hadi siku, kwa kuzingatia matukio ya Asia Magharibi, amewataka viongozi wa Wamagharibi waonyeshe umoja wao waliouonyesha katika kuiunga mkono Israel dhidi ya Iran hivi karibuni, kwa kuipa Kyiv silaha na vifaa zaidi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Moscow.

Katika kujibu ombi la Zelensky kwa nchi za Magharibi la kuiweka Ukraine katika ngazi moja ya usalama na Israel, Ikulu ya Marekani imetoa jibu la  kukatisha tamaa katika uwanja huo. Msemaji wa Usalama wa Taifa wa White House John Kirby, akizungumzia ushiriki wa Marekani katika kuilinda Tel Aviv dhidi ya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, amesema kuwa Washington haitachukua hatua kama hilo kwa Kyiv katika vita vyake na Russia. Kuhusiana na suala hilo hadi sasa Warepublican wa Baraza la Wawakilishi la Marekani wamekuwa wakizuia kuidhinisha mswada wa misaada ya kigeni uliopendekezwa na Rais Joe Biden wa Marekani mnamo Oktoba 2023.

Kwa utaratibu huo, mtazamo wa vita vya Ukraine katika mwaka wake wa tatu hautakuwa na matumaini yoyote kwa rais huyo mwenye mwelekeo wa Kimagharibi katika suala la kushinda vita hivyo au kukomboa tena maeneo yaliyo mkononi mwa Russia. Ukweli ni kwamba, Waukraine waliingia katika mzozo mkubwa na Russia  kwa ushawishi na uchochezi wa Magharibi, lakini sasa wamewapa mgongo. Hii ni pamoja na kuwa, utabiri wa maafisa wakuu wa nchi za Magharibi kuhusu matokeo ya vita vya Ukraine unaikatisha tamaa kabisa Kyiv. William Burns, Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ameonya kuhusu kushindwa Ukraine katika vita na Russia. Huku akiashiria kiwango kidogo cha vifaa vya vita kwa  jeshi la Ukraine, Burns amesema: "Kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa Ukraine mwaka huu, lakini misaada zaidi ya kijeshi ya Marekani katika uwanaj huo inaweza kuwa na manufaa kwa nchi hiyo."

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China