Rais Raisi: Israel ikifanya kosa jengine dogo haitabaki tena
Get link
Facebook
X
Pinterest
Email
Other Apps
-
Apr 24, 2024 02:45 UTC
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran amesema katika kikao na wasomi wa jimbo wa Punjab nchini Pakistan
kwamba iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utafanya kosa jengine dogo na
kuivamia ardhi takatifu ya Iran, hali itakuwa tofauti kabisa na hakuna
ajuaye kama utawala huo utabaki tena.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran IRIB, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake nchini
Pakista, Ebrahim Raisi jana alitembelea Chuo Kikuu cha "GCU" cha Lahore
na kukutana na wasomi wa kielimu na kitamaduni wa jimbo la Punjab.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliieleza hadhara ya wasomi hao
kwamba, taifa kubwa la Iran liliutia adabu utawala wa Kizayuni kwa
jinai ya kushambulia sehemu ya ubalozi wake nchini Syria, kitendo
ambacho ni kinyume cha sheria zote za kimataifa, mikataba na Hati ya
Umoja wa Mataifa na akaongeza kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utafanya
kosa jengine dogo tu, hautabaki tena.
Seyyid Raisi amesema, madai ya Wamagharibi kwamba eti wanatetea haki
za binadamu hayana ukweli, kama yalivyo madai yao ya kuunga mkono
uhuru wa fikra, na akaongeza kuwa, uungaji mkono wa Marekani na
Magharibi kwa mauaji na kujeruhiwa zaidi ya Wapalestina 100,000 katika
Ukanda wa Ghaza ni ithbati ya ukweli kwamba leo hii wavunjaji wakubwa wa
haki za binadamu ni Wamarekani na Wamagharibi, na madai yao ya kutetea
haki za binadamu ni upuuzi tu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilevile ameeleza furaha
aliyonayo kwa kutembelea mji wa kihistoria, kiutamaduni na wa kuvutia wa
Lahore na akasema, uhusiano wa Iran na Pakistan, mbali na kuwa ni wa
ujirani, zaidi ni wa kidini, kiutamaduni, kiustaarabu na wa kinyoyo,
ambao umepelekea kuwepo mfungamano usioweza kuvunjika kati ya mataifa
hayo mawili.
Kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Pakistan, Rais Ebrahim Raisi wa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumatatu alielekea Islamabad, mji
mkuu wa nchi hiyo, akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na
kiuchumi kwa ajili ya ziara ya siku tatu nchini humo.../