Rais wa Iran anaitembelea Pakistan siku ya Jumatatu
Tangazo kutoka wizara ya mambo ya nje ya Islamabad lilisema ziara hii itatoa fursa muhimu kuimarisha uhusiano wa nchi mbili
Rais wa Iran Ebrahim Raisi atawasili katika nchi jirani ya Pakistan Jumatatu kwa ajili ya mikutano rasmi na viongozi wa taifa hilo huku kukiwa na mivutano kati ya Iran na Israel.
Tangazo kutoka wizara ya mambo ya nje ya Islamabad leo Jumapili lilisema kuwa mazungumzo hayo yatatoa fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na ushirikiano katika biashara, mawasiliano, nishati, na kilimo.
Tangazo lilisema ujumbe wa ngazi ya juu wa Raisi utawajumuisha waziri wa mambo ya nje wa Iran, mawaziri wengine na wawakilishi wa biashara. Wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Pakistan, rais wa Iran anatarajiwa kukutana na mwenzake, Asif Ali Zardari, na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, miongoni mwa wengine.
Taarifa ya Pakistan imesema bila kufafanua, pia watajadili maendeleo ya kikanda na kimataifa na ushirikiano wa nchi hizi mbili ili kupambana na tishio la pamoja la ugaidi.