Al-Qassam: Tumeangamiza na kukamata mateka askari kadhaa wa Kizayuni + Video
Abu Obeida, Msemaji wa Brigedi za Izzuddinul-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ametangaza kuwa, wapiganaji wa brigedi hizo wamekinasa kwa kukiwekea chambo chini ya handaki kikosi cha jeshi la Kizayuni na kufanikiwa kuwaangamiza, kuwajeruhi na kuwakamata mateka askari kadhaa wa jeshi hilo katika eneo la kambi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.
Abu Obeidah, ameonyesha mkanda wa video wa operesheni hiyo
iliyotekelezwa na Muqawama na kutangaza kuwa jana Jumamosi jioni katika
kambi ya Jabalia, wapiganaji wa Kipalestina waliwawekea chambo wanajeshi
wa Israel kilichowaingiza kwenye moja ya mahandaki na kufanikiwa
kuwaangamiza na kuwajeruhi askari kadhaa, mbali na wengine waliowakamata
mateka.
Kufuatia kutangazwa habari hiyo ya kukamatwa mateka wanajeshi
kadhaa wa utawala huo ghasibu wa Kizayuni huko Ghaza, furaha, nderemo na
vifijo vilitawala jana usiku katika miji ya Dura na Sour na kwenye
kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Ain Al-Hilweh na Nahr al-Bared
zilizoko nchini Lebanon na katika kambi zingine kadhaa.
Katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pia, sauti za Takbira zilisikika kutoka kwenye vipaza sauti vya misikiti zilizowataka pia watu wamiminike mitaani kusherehekea ushindi huo.
Japokuwa kama ilivyokuwa huko nyuma jeshi la utawala bandia wa
Israel lilikanusha haraka tukio hilo, msemaji wa Izzuddinul-Qassam
alitoa mkanda wa video wa operesheni hiyo iliyotekelezwa na wapiganaji
wa Muqawama iliyoonyesha pia silaha na zana zilizonaswa kutoka kwa
wanajeshi wa Israel.
Mwanachama huyo mwandamizi wa Hamas amebainisha pia kuwa tangu wiki
mbili zilizopita, makumi ya operesheni za kijeshi zimetekelezwa dhidi
ya jeshi vamizi la Kizayuni huko Rafah na Beit Hanoun, wakati jeshi hilo
linajaribu kuwaonyesha Wazayuni kwamba "kufukua makaburi" ya maiti za
Wapalestina huko Ghaza ni mafanikio ya kijeshi na kimaadili ambayo
limepata katika eneo hilo.../