Biden airuhusu Ukraine ishambulie maeneo ya Russia kwa silaha za Marekani, aikasirisha Moscow
Rais Joe Biden wa Marekani amelegeza marufuku aliyokuwa ameiwekea Ukraine na kuiruhusu kutumia silaha za Washington kushambulia ndani ya ardhi ya Russia ili kuisaidia kulinda eneo lake la kaskazini mashariki la Kharkiv dhidi ya mashambulizi.
Uamuzi huo unaashiria mabadiliko ya sera ya Biden ambaye awali alikataa kuiruhusu Kyiv kutumia silaha za Marekani nje ya mipaka ya Ukraine, na unachukuliwa huku Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya zikidokeza kuwa zitairuhusu Ukraine kutumia silaha zao kulenga maeneo ya kijeshi ndani ya ardhi ya Russia.
Kwa uamuzi huo, Kyiv itaidhinishwa kushambulia maeneo ya kijeshi kwenye mpaka na mkoa wa Kharkiv, ambao vijiji vyake kadhaa vilitekwa na Russia tangu Mei 10 na kuwafanya maelfu ya watu walazimike kuyahama makazi yao.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Vladimir Putin wa Russia alionya siku ya Jumanne juu ya alichokiita "matokeo hasi makubwa", akisisitizia nguvu na uwezo wa nyuklia wa nchi yake, endapo washirika wa Magharibi wa Ukraine watalegeza sera zao za awali.
Wakati huohuo Shirika la habari la RIA la Russia limemnukuu Andrei Kartapolov, mkuu wa kamati ya ulinzi ya Bunge la Chini akisema kuwa, Moscow italipiza kisasi kwa njia isiyo na mlingano kwa mashambulizi ya Ukraine dhidi ya ardhi yake kwa kutumia silaha zinazotolewa na Marekani.
Kartapolov amesisitiza kuwa uamuzi wa Biden wa kuruhusu mashambulizi ya makombora yenye mpaka maalumu kufanywa ndani ya ardhi ya Russia kwa kutumia silaha za Marekani hautaathiri operesheni ya kijeshi ya Moscow nchini Ukraine.../