Israel yamaliza mashambulizi ya wiki tatu kaskazini mwa mji wa Gaza
Vikosi vya Israel vimeondoka Jabalia kaskazini mwa Gaza, baada ya mashambulizi ya wiki tatu eneo hilo ambayo yalishuhudia makumi ya maelfu ya raia wakitoroka.
Jeshi lilisema "mamia ya magaidi [wameondolewa]" na kilomita 10 za mahandaki ziliharibiwa wakati wa operesheni hiyo.
Picha kutoka Jabalia zinaonyesha uharibifu mkubwa, huku majengo ya orofa mbalimbali yakiwa yameharibiwa au kulipuliwa kwa mabomu.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vilikuwa vimerejea mjini humo miezi kadhaa baada ya kujiondoa, vikisema kuwa Hamas inajipanga tena huko.
Wakati wa operesheni hiyo, miili saba ya Waisraeli waliouawa wakati wa shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba na kupelekwa Gaza iligunduliwa na kurejeshwa makwao.
Gazeti la Times la Israel lilisema maafisa wa IDF wameelezea mapigano ya Jabalia kama baadhi ya vita vikali zaidi.
IDF ilisema Hamas "imegeuza eneo la kiraia kuwa ngome ya mapigano, iliyofyatuliwa risasi kuelekea upande wa wanajeshi kutoka maeneo ya kujihifadhi na shule, na kujenga mtandao wa kigaidi wa chini ya ardhi kutoka ndani ya majengo ya kiraia".
IDF ilisema iliharibu virusha roketi vilivyokuwa "tayari kwa matumizi" na maeneo kadhaa ya kutengeneza silaha.
Operesheni ya pili ya IDF ya ardhini huko Jabalia ilifanyika miezi minne baada ya kutangaza kuwa imesambaratisha uwezo wa kijeshi wa Hamas kaskazini mwa Gaza.