Je, Trump anaweza kugombea urasi baada ya kukutwa na hatia?
Donald Trump amekuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kuhukumiwa kwa mashtaka ya jinai, baada ya jopo maalum la mahakama mjini New York kumpata na hatia katika mashtaka yote 34 dhidi yake.
Mashtaka hayo yote yanahusiana na kughushi rekodi za biashara yake ili kuficha malipo aliyolipwa nyota wa zamani wa filamu za ngono Stormy Daniels ili kumshurutisha kutosema lolote kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2016.
Sasa ni nini kitafuata baada ya uamuzi huu?
Haya hapa ni baadhi ya masuala muhimu ya kuzingatia.
Bado anaweza kugombea urais?
Ndio. Katiba ya Marekani inaweka masharti machache ya kustahiki kwa wagombeaji urais: lazima wawe na angalau miaka 35, wawe raia wa Marekani "wazaliwa asili" na wameishi Marekani kwa angalau miaka 14. Hakuna sheria zinazozuia wagombea walio na rekodi za uhalifu.
Lakini uamuzi huu wa hatia bado unaweza kuathiri uchaguzi wa urais wa Novemba. Kura ya maoni kutoka kwa Bloomberg na Morning Consult mapema mwaka huu iligundua kuwa 53% ya wapiga kura katika majimbo muhimu yanayoweza kuamua mshindi wa uchaguzi wangekataa kumpigia kura mgombea wa Republican ikiwa atapatikana na hatia.
Kura nyingine ya maoni, kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac mwezi huu, ilionyesha 6% ya wapiga kura wa Trump wangekuwa na uwezekano mdogo wa kumpigia kura - hatua ambayo itaathiri matokeo katika kinyang'anyiro kikali kama hicho.
Trump atafanya nini sasa?
Trump amekuwa huru kwa dhamana wakati wote wa kesi na hili halikubadilika baada ya hukumu kusomwa siku ya Alhamisi - Mrepublican huyo aliachiliwa kwa kujitambua kwake.
Atarejea kortini tarehe 11 Julai - tarehe ambayo Hakimu Juan Merchan amepanga kusikilizwa kwa hukumu.
Jaji atakuwa na mambo kadhaa ya kuzingatia katika hukumu, ikiwa ni pamoja na umri wa Trump.
Hukumu hiyo inaweza kuhusisha faini, muda wa majaribio au usimamizi, au pengine kifungo.
Trump, ambaye aliita uamuzi huo kuwa wa "fedheha", bila shaka atakata rufaa, mchakato ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa au hata zaidi.
Mawakiliwake watakabiliana na Kitengo cha Rufaa huko Manhattan, na ikiwezekana Mahakama ya Rufaa.
Hii yote ina maana kwamba hata baada ya kuhukumiwa itakuwa vigumu sana Trump aondoke mahakamani akiwa amefungwa pingu, kwani angetarajiwa kusalia huru kwa dhamana huku akikata rufaa.