Jeshi la Yemen latungua ndege ya kivita ya Marekani isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper
Msemaji wa Jeshi la Yemen (YAF) ametangaza kuwa, vitengo vya ulinzi wa anga vya nchi hiyo vimefanikiwa kuangusha ndege ya kivita isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper ilipokuwa katika operesheni za uhasama katika anga ya mkoa wa kati wa Bayda.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema katika taarifa siku ya Jumanne kwamba ndege hiyo isiyo na rubani, ambayo ni ya kisasa kabisa, ililengwa kwa kombora la kutoka ardhini hadi angani, na kwamba picha za operesheni hiyo zitatolewa baadaye.
Kwa mujibu wa Jenerali Saree, hii ni ndege ya tano ya aina hiyo ambayo walinzi wa anga wa Yemen wameiangusha tangu kuanza kwa operesheni za kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza ambao wanakabiliwa na vita vya mauaji ya halaiki ya utawala wa Israel.
Msemaji huyo amethibitisha kuwa Wanajeshi wa Yemen wataendelea kuimarisha uwezo wao wa ulinzi ili kukabiliana na uvamizi wa pamoja wa Marekani na Uingereza dhidi ya nchi yao, na wataendelea na operesheni zinazoiunga mkono Palestina hadi uvamizi na mzingiro wa pande zote wa Israel dhidi ya Gaza utakapokoma kikamilifu.
Ndege moja isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper ya Marekani inagharimu takribani dola milioni 30 na ina uwezo wa kubeba makombora manane na ina uwezo wa kuruka hadi fiti 50,000 juu kwa muda wa masaa 24.