Kamati Kuu ya kuchunguza ajali ya helikopta iliyombeba Shahidi Ebrahim Raisi yatoa ripoti ya pili

 

May 30, 2024 03:40 UTC
  • Kamati Kuu ya kuchunguza ajali ya helikopta iliyombeba Shahidi Ebrahim Raisi yatoa ripoti ya pili

Kituo cha Mawasiliano cha Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimetoa ripoti ya pili ya Kamisheni Kuu ya kuchunguza sababu za ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha Rais Seyed Ebrahim Raisi, na ujumbe ulioandamana naye.

Helikopta iliyokuwa imembeba Rais Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Amir-Abdollahian, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Tabriz Ayatullah Mohammad Ali Al-e-Hashem, Gavana wa Azarbaijan Mashariki Malek Rahmati, kamanda wa kikosi cha walinzi wa rais, marubani wawili na walinzi ilianguka mkoa wa kaskazini-magharibi wa Azarbaijan Mashariki mnamo Mei 19, 2024. Miili yao ilipatikana siku ya Jumatatu baada ya msako wa usiku mzima katika eneo lililokuwa na hali mbaya ya hewa. Wote waliokuwamo ndani ya helikopta hiyo walipoteza maisha na kupata daraja ya juu ya kufa shahidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya pili iiliyotangazwa Jumatano na Kamati Kuu ya Kuchunguza Sababu za Ajali ya Helikopta iliyombeba Rais na ujumbe aliofuatana nao, sehemu kubwa ya nyaraka zinazohusiana na ukarabati na matengenezo ya helikopta iliyoanguka zilichunguzwa kwa makini na hakuna matatizo yoyote yaliyobainika. Aidha helikopta hiyo ilikuwa imebeba abiria kwa mujibu wa uwezo wake. 

Shahidi Rais Ebrahim Raisi na mashahidi wenzake katika ajali ya helikopta

Halikadhalika kulingana na mazungumzo ya mwisho yaliyorekodiwa kati ya marubani wa helikopta katika msafara na helikopta iliyoanguka hakuna tangazo la dharura lililorekodiwa.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa hakuna mlipuko wowote uliotokea wakati helikopta ikiwa inaruka na kabla ya kugonga mlima.

Pia imeelezwa katika ripoti kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wa kitaalamu hakuna athari za vita vya kielektroniki kwenye helikopta iliyoanguka.

Ripoti ya awali ya Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisema  uchunguzi wao wa awali umebaini kuwa, hakuna kitu chochote kisichokuwa cha kawaida kinachoweza kuhusishwa na ajali ya helikopta ya rais iliyoanguka. Ripoti hiyo ya wiki iliyopita ilibainisha kuwa; "Hakuna alama zozote za kuashiria kuwa helikopta hiyo ilitunguliwa au kushambuliwa." Uchunguzi wa sababu ya kuanguka helikopta hiyo ungali unaendelea

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo