Larijani na Jalili wajiandikisha kugombea urais Iran
Zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kuwania urais katika uchaguzi wa mapema mwezi ujao nchini Iran, limeingia siku ya pili leo ambapo wanasiasa mashuhuri wamejiandikisha kuchukua nafasi ya urais kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raeisi katika ajali ya helikopta.
Saeed Jalili, mjumbe mkuu wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran alikuwa mwanasiasa wa kwanza mwenye uzito kujiandikisha siku ya Alhamisi kwa ajili ya uchaguzi huo.
"Maendeleo ya watu wetu na mielekeo ya kimataifa yanaonyesha kwamba tunakabiliwa na fursa ya kihistoria," alisema baada ya usajili huo, akiashiria hapo kukiri maafisa wa Marekani kwamba sera yao ya "mashinikizo ya juu" dhidi ya Iran imeshindwa.
Mapema leo Ijumaa pia, spika wa zamani wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Ali Larijani amefika katika Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani na kujiandikisha kuwania nafasi ya urais. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujiandikisha, Larijani, ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia amesema matatizo ya nchi yanaweza kutatuliwa kwa kutegemea uwezo wa ndani na kutumia uzoefu wa kimataifa. Larijani na Jalili hivi sasa ni wajumbe katika Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu,
Kipindi cha siku tano cha kujiandikisha kugombea urais kilichoanza Alhamisi kitashuhudia wale walio na umri wa kati ya miaka 40 hadi 75 wakiwa na angalau shahada ya uzamili wakijiandikisha kama wagombea wanaotarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa urais wa Juni 28.
Wagombea wote hatimaye lazima waidhinishwe na Baraza la Walinzi wa Katiba la Iran lenye wanachama 12, jopo ambalo hukagua sifa za watarajiwa mbali na kusimamia zoezi zima la uchaguzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi amesema mchakato wa kuwachunguza waliojiandikisha utadumu kwa siku saba na kisha wagombea waliofuzu watakuwa na karibu wiki mbili za kufanya kampeni za uchaguzi. Baraza la Walinzi litachapisha orodha ya wagombea waliohitimu mnamo Juni 11