Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma atikisa chama tawala ANC
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesababisha athari kubwa katika uchaguzi huu.
Chama chake kipya, uMkonto weSizwe (MK), kimepata kura kutoka kwa wafuasi wa African National Congress (ANC), na kupunguza wingi wa wabunge ANC.
Kinafanya vizuri kiasi kwamba kwa sasa kiko katika nafasi ya tatu - mbele ya Economic Freedom Fighters (EFF).
Ukuaji wa chama cha MK ni wa ajabu. Kiliandikishwa tu Septemba iliyopita, huku Bw Zuma mwenye umri wa miaka 82, mwanachama wa ANC tangu akiwa na umri wa miaka 17, akitangaza mnamo Desemba kwamba anajiunga nacho kwani hangeweza kupigia kura chama cha ANC kinachoongozwa na Ramaphosa.
Tangu wakati huo, chama cha MK kimetikisa siasa za Afrika Kusini kwa namna ambayo hakuna chama kingine kimewahi kufanikiwa kiasi hicho katika kipindi kifupi mno - tangu kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi miaka 30 iliyopita.
Na Bw. Zuma amefanikisha hili licha ya kwamba ni mhalifu aliyehukumiwa na kuzuiwa kuchukua kiti katika bunge jipya.
Alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela kwa kosa la kudharau baada ya kukaidi agizo la mahakama la kufika mbele yake juu ya uchunguzi kuhusu ufisadi katika kipindi chake cha urais kwa miaka tisa.
Aliachiliwa na Rais Cyril Ramaphosa baada ya kutumikia miezi mitatu ya kifungo chake.
Bw Ramaphosa analazimika kujutia uamuzi huo kwani Bw. Zuma sasa amekitikisa chama chake - ANC - katika uchaguzi huo.