Ufilipino yaionya China dhidi ya 'vitendo vya vita'
Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr ameionya China kutovuka mstari mwekundu katika suala la Bahari ya China Kusini, ambako mzozo kati ya nchi hizo mbili unaendelea kushika kasi.
Iwapo mfilipino yeyote atafariki kutokana na hatua za makusudi za Uchina, alisema, Ufilipino ingeichukulia kuwa karibu na "kitendo cha vita" na kujibu ipasavyo.
Bw. Marcos alikuwa akizungumza katika kongamano la usalama nchini Singapore lililohudhuriwa na wakuu wa ulinzi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, zikiwemo Marekani na China.
Kujibu, msemaji wa jeshi la Uchina aliishutumu Ufilipino kwa "kuelekeza lawama kwa Uchina" na "kuishambulia kwa maneno".
Katika miezi ya hivi karibuni mzozo wa muda mrefu kati ya China na Ufilipino kuhusu eneo katika Bahari ya China Kusini umeongezeka.
Ufilipino imelalamika vikali kuhusu meli za kushika doria za China kurusha maji ya kuwasha kwenye boti za Ufilipino na meli za upelekaji bidhaa nchini humo huku Beijing ikisema inatetea uhuru wake.