UN inakosolewa kwa kutoa heshima zake kwa Rais wa Iran Hayati Ebrahim Raisi
Napenda kuwahakikishia kuwa Umoja wa Mataifa unasimama katika mshikamano na watu wa Iran, anasema Antonio Guterres
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limekosolewa Alhamisi kwa kutoa heshima zake kwa rais wa zamani wa Iran, Ebrahim Raisi aliyefariki katika ajali ya helikopta, huku Marekani ikisusia mkutano huo. Kufuatia ukimya wa dakika moja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa tukio la Mei 19, pamoja na watu wa Iran.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Umoja wa Mataifa unasimama katika mshikamano na watu wa Iran na katika harakati za kutafuta amani, maendeleo, na uhuru wa kimsingi”, alisema Guterres. “Kwa hiyo, Umoja wa Mataifa utaongozwa na Mkataba wa kusaidia kutambua amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa wote,” aliongeza.
Alipoulizwa kuhusu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kutoa rambirambi siku chache baada ya kifo cha kiongozi huyo, msemaji rasmi wa Guterres aliutetea msimamo wake. Katibu Mkuu hajawahi kuwa na aibu kuelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya hali ya haki za binadamu nchini Iran, hasa juu ya masuala ya wanawake, Stephane Dujarric alisema.
“Haimzuii kutoa rambirambi wakati mkuu wa nchi mwanachama wa shirika hili, na waziri wa mambo ya nje, ambaye alikutana naye mara kwa mara, amefariki katika ajali ya helikopta,” aliongeza.