"Vitisho vya nyuklia vya Israel vitabadilisha mlingano wa usalama katika eneo"
Katibu wa Baraza la Kistratajia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesema vitisho vinavyotolewa na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel vya kutumia silaha za nyuklia huenda vikawalazimisha wengine kuangalia upya sera zao za nyuklia katika eneo la Asia Magharibi.
Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana katika warsha iliyoandaliwa na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar mjini Doha, chini ya kaulimbiu 'Mlingano baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa katika kiwango cha kieneo.'
Amebainisha kuwa, maafisa wapenda vita wa utawala wa Kizayuni si tu wanabwabwaja na kutoa vitisho kuhusu kutumia mabomu ya atomiki, lakini si baidi wakaisukuma Tel Aviv itekeleza kivitendo vitisho hivyo.
Araqchi ameuambia mkuatano huo mjini Doha kuwa, Israel haijawahi kukiri au kukanusha madai kuwa inamiliki silaha za nyuklia, na hilo linaonesha namna utawala huo una sera fiche na zisizoeleweka. "Hata hivyo maafisa wa Israel wamelazimika kubadilisha stratejia yao tangu vita vya Gaza vianze," ameongeza Araqchi.
Mwanadiplomasia huyo wa wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, eneo la Asia Magharibi linapasa kuwa huru kutokana na silaha za nyuklia, na kwamba utawala wa Kizayuni unapasa kupokonywa silaha hizo za atomiki.
Kadhalika Katibu wa Baraza la Kistratajia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amekosoa vikali matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Seneta wa Marekani, Lindsey Graham ya kuutaka utawala wa Kizayuni utumie mabomu ya nyuklia dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Mgombea huyo wa chama cha Republican katika jimbo la South Carolina alipendekeza kuwa Israel itakuwa sawa kusambaratisha kikamilifu Ukanda wa Gaza uliozingirwa.