Wako wapi watu 13,000 waliopotea Gaza wakati wa mashambulizi ya Israel?
Israel?
Wakati idadi ya watu waliouawa huko Gaza inaendelea kuongezeka, idadi hii haijumuishi waathiriwa wapatao 13,000 ambao wamepotea.
Wengi wao wamefunikwa chini ya vifusi, lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wengine huenda wamechukuliwa kwa nguvu.
Ahmed Abu Duke amekuwa akimtafuta kaka yake Mustafa kwa miezi kadhaa.
Familia hiyo ilikuwa imejihifadhi katika eneo la Hospitali ya Nasser, katika mji wa kusini wa Khan Yunis, wakijaribu kuepuka mashambulizi ya Israel.
Lakini walipopata habari kwamba nyumba yao, imeteketezwa na moto, Mustafa alikwenda kuangalia sehemu ya mabaki ya nyumba na mali. Ila hakurudi tena.
"Tulitafuta kila sehemu," anasema Ahmed, akielezea eneo palipokuwa na nyumba, sasa kuna mabaki ya vitu vyeusi vilivyoungua.
"Eneo la jirani limeharibiwa na majengo ya ghorofa yamebomolewa," anasema.
Familia ilimtafuta Mustafa, dereva mstaafu wa gari la wagonjwa, miongoni mwa miili ambayo kikosi cha Ulinzi wa Raia, kinachoongozwa na Hamas kiliopoa kutoka kwenye vifusi na makaburi ya halaiki, lakini hawakuweza kumpata.
"Bado tunatumai tutampata katika gari la wagonjwa linalowasili hospitalini," anasema Ahmed.
Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema idadi ya watu waliouawa katika mzozo huu hadi sasa inazidi 35,000, takwimu hizi zinajumuisha vifo vilivyorekodiwa hospitalini tu.
Euro-Med Human Rights Monitor, shirika la haki za binadamu lisilo la kiserikali lenye makao makuu mjini Geneva, linakadiria watu 13,000 wametoweka tangu vita kuanza na kupotea bila ya kujulikana walipo.
Takwimu hizi hazitofautishi kati ya raia na wapiganaji wa Hamas, kundi ambalo lilianzisha mashambulizi ya kuvuka mpaka dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba na takribani watu 1,200 waliuwawa na 252 walichukuliwa mateka.
Israel ilijibu kwa kampeni kubwa ya kijeshi huko Gaza.
Ukubwa wa vifusi
Kuna familia nyingi, kama za Mustafa, ambazo hazina uhakika kuhusu nini kimetokea kwa wapendwa wao waliopotea katika kipindi cha miezi saba iliyopita.
Timu ya Ulinzi wa Raia wa Gaza, ambayo ni sehemu ya idara za usalama za Mamlaka ya Palestina, inakadiria zaidi ya watu 10,000 kati yao huenda wamefukiwa chini ya vifusi.
Umoja wa Mataifa unakadiria kiasi cha vifusi katika Ukanda wa Gaza ni karibu tani milioni 37, na miili mingi ya watu imefukiwa na kuna takribani tani 7,500 ya silaha ambazo hazijalipuka. Jambo linalowaweka hatarini waokoaji na watu wa kujitolea.
Ulinzi wa Raia unasema timu zake hufanya kazi na watu wa kujitolea kutoa miili kutoka chini ya vifusi, lakini wanatumia zana duni na mara nyingi ni vigumu kuwafikia waliokufa.
Pia kuna wasiwasi, kuacha miili bila kuitoa na kuoza, wakati Gaza inaelekea katika miezi yake ya joto, kunaweza kusababisha maafa ya kiafya.
Abdul Rahman Yaghi pia anakumbana na changamoto anapojaribu kuwatoa jamaa zake kutoka kwenye vifusi.
Nyumba ya ghorofa tatu ya familia yake katika mji wa kati wa Gaza wa Deir Al-Balah ilipigwa na kombora mwezi Februari 22 huku watu 36 wa familia yake wakiwa ndani.
Miili 17 ilipatikana, lakini baadhi ya sehemu za miili, ambazo zilipatikana, hazijatambuliwa.
“Bado hatujapata mingi ya miili ya watoto waliokuwa ndani ya nyumba hiyo,” anasema.
Ulinzi wa Raia umeomba msaada wa kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa na nchi zilizo na timu zenye uzoefu kusaidia kuondoa miili hiyo.
Walitoa wito kwa mashirika ya kimataifa "kuingilia kati mara moja" na kuishinikiza Israel kuruhusu vifaa vizito kuingia Gaza kusaidia juhudi za uokoaji, lakini anasema bado hajapata jibu.
Amnesty International inaamini watu wengine ambao wametoweka, wanaweza kuwa wamezuiliwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), bila familia zao kujua, wakiita ni "kuchukuliwa kwa nguvu."
Euro-Med Human Rights Monitor inakadiria mamia ya Wapalestina huko Gaza wanashikiliwa na IDF bila familia zao kufahamishwa.
Mikataba ya Geneva, ambayo Israel imetia saini, inaeleza nchi lazima iripoti utambulisho na eneo la raia wanaozuiliwa.
Serikali ya Israel ilisitisha ziara za Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), katika kambi za vizuizi kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7.
Hisham Muhanna, wa ICRC huko Gaza, anasema "ameomba mara kwa mara kuonana na wafungwa wa Kipalestina, lakini kamati hiyo bado haijaruhusiwa kuwaona."
ICRC inaongeza kuwa, haijaruhusiwa pia kuwatembelea mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas.
BBC iliwasiliana na IDF kupata majibu lakini haikujibu chochote.
Tumaini
Katika mji wa al-Zawaida katikati mwa Gaza, familia nyingine inamtafuta mtoto wao wa kiume aliyetoweka. Wana hofu huenda akawa ni miongoni wa waliochukuliwa kwa nguvu.
Akiwa na picha yake mkononi, mamake Mohamed Ali alimtafuta hadi pale mtu alipomwambia anashikiliwa na IDF. Mtu huyo anasema Mohamed alikuwa hai mara ya mwisho alipomwona, lakini hawajui nini kimempata tangu wakati huo.
Mohamed alitoweka tangu Disemba 23, wakati familia hiyo ilipoondoka nyumbani kwao na kukimbilia katika shule ya Jabalia, kaskazini mwa Gaza, wakati wa mashambulizi makali ya Israel.
Lakini wanajeshi wa Israel waliingia shuleni hapo na kuwaamuru wanawake na watoto kuondoka, anasema mke wa Mohamed, Amani Ali.
Anaongeza kuwa wanaume wote walirudi katika familia zao usiku huo, isipokuwa Mohamed.
Mahali alipo na kilichompata hakijulikani.
Amani anasema hajui ikiwa afikirie mumewe amekufa au amezuiliwa na IDF. Anasema hilo linampa matumaini kuwa yu hai.
“Kama atakuwa hai na huru, atatutafuta na kutupata,” anasema Amani.
Wizara ya Afya iliunda fomu ya mtandaoni kwa jamaa za waliofariki na waliopotea kujaza ili kupata taarifa zaidi na za kina juu ya kile kilichotokea kwa wale waliotoweka tangu Oktoba 7.
Hadi wakati huu, familia nyingi zitaendelea kuwatafuta wapendwa wao.