Wataalamu zaidi ya 50 wa UN wataka Israel iwekewe vikwazo na marufuku ya silaha
Wataalamu zaidi ya 50 wa Umoja wa Mataifa wametoa mwito wa kuchukuliwa "hatua madhubuti kimataifa" baada ya kuelezea walivyokasirishwa na shambulio la kinyama la jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ambalo liliua Wapalestina wasiopungua 45 waliokuwa wametafuta hifadhi kwenye kambi ya muda huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Wataalamu hao wa UN wamesema: "picha za kutisha za uharibifu,
watu kubaki bila makazi na vifo zimeibuka kutoka Rafah, zikiwemo za
watoto wachanga walioraruliwa vipandevipande na watu kuteketezwa wakiwa
hai".
Kundi hilo la wataalamu zaidi ya 50 wa Umoja wa Mataifa limeendelea
kueleza katika taarifa yake kwamba, ripoti zilizotoka kwenye eneo
lililolengwa zinaonyesha kuwa shambulio la jeshi la Kizayuni lilikuwa la
kiholela na lisilo na mlingano, na lilifanywa wakati watu wakiwa
wamekwama ndani wakiungua kwenye mahema ya plastiki, na kusababisha vifo
vya kutisha.
![](https://media.parstoday.ir/image/4c6da9e1c718132hz9d_800C450.jpg)
Wataalamu hao wa UN wamebainisha kuwa, mashambulizi hayo "ya kinyama"
yanaingia kwenye kundi la ukiukaji mkubwa wa sheria za vita, na
wakaongeza kuwa wao kwa upande wao wamefadhaishwa sana na jinsi jamii ya
kimataifa ilivyoshindwa kukomesha mashambulizi ya Israel dhidi ya
Ghaza.
Wataalamu hao wametaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu shambulio la
Rafah, sambamba na kuchukuliwa hatua za haraka za kuuwekea utawala wa
Kizayuni wa Israel vikwazo na marufuku ya silaha.
Aidha wamesema, kueleza kuwa shambulio la Rafah lilifanywa 'kimakosa'
hakulifanyi liwe halali wala hakuwarejeshi waliouawa au kuwafariji
manusura.
Kundi hilo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limemalizia taarifa yake kwa
kusema: "machungu ya watu wa Ghaza lazima yakomeshwe hivi sasa
hivi".../