Watu 11 wauawa katika shambulizi la Urusi nchini Ukraine

 .

Takriban watu 11 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya Urusi kushambulia duka kubwa katika mji wa kaskazini mwa Ukraine wa Kharkiv kwa mabomu mawili ya kuteleza, maafisa wa eneo hilo wamesema.

Moto mkubwa ulionekana ukiwaka kwenye duka moja nje kidogo ya kaskazini mwa jiji.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema zaidi ya watu 200 huenda walikuwa ndani ya duka hilo kubwa wakati liliposhambuliwa.

Siku ya Jumapili, gavana wa Kharkiv Oleh Syniehubov alisema idadi ya vifo imeongezeka hadi 11.

Hapo awali alikuwa amesema watu sita "walifariki papo hapo", wengine 40 walijeruhiwa huku 16 wakiwa hawajulikani waliko.

Meya wa Kharkiv Ihor Terekhov alisema: "Idadi kubwa ya watu hawapo. Huu ni ugaidi mtupu."

Rais Zelensky aliongeza: "Shambulizi dhidi ya Kharkiv ni dhihirisho lingine la wazimu wa Urusi.

"Ni wendawazimu tu kama [Rais wa Urusi Vladimir] Putin wana uwezo wa kuua na kuwatisha watu kwa njia hii."

Shambulizi la pili katikati mwa Kharkiv baadaye Jumamosi lilijeruhi watu wanane, kulingana na Bw Terekhov.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo