Watu weusi walishtaki shirika la ndege, American Airlines kwa ubaguzi wa rangi

Kutoka kushoto: Alvin Jackson, Emmanuel Jean Joseph na Xavier Veal

Wanaume watatu weusi wamewasilisha kesi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya shirika la ndege la American Airlines, wakidai kuwa ndege hiyo iliwaondoa kwa muda kutoka kwa ndege baada ya malalamiko kuhusu harufu ya mwili.

Wanaume hao, ambao hawakuketi pamoja na hawakujuana, wanasema kuwa kila mtu mweusi aliondolewa kwenye ndege ya Januari 5 kutoka Phoenix, Arizona, hadi New York.

"American Airlines ilitutenga kwa kuwa watu Weusi, ilituaibisha, na ilitudhalilisha," watu hao walisema katika taarifa ya pamoja siku ya Jumatano.

Shirika hilo la ndege lenye makao yake makuu Texas, lilisema kuwa linachunguza suala hilo kwani madai hayo hayaendani na maadili yake.

Kulingana na kesi iliyowasilishwa na kundi la kutetea wateja la Public Citizen, watu hao walikuwa tayari wameketi na walikuwa wakijiandaa kuondoka Phoenix wakati mhudumu wa ndege alipomwendea kila mmoja wao na kuwataka watoke nje ya ndege.

Alvin Jackson, Emmanuel Jean Joseph, na Xavier Veal wanadai kuwa, walipokuwa wakiondoka, waligundua kuwa "kila mtu Mweusi kwenye ndege alikuwa akiondolewa".

Kila mmoja alisafiri kwa ndege kutoka Los Angeles mapema siku hiyo, bila shida yoyote. Katika lango la ndege, wanaume hao watatu, pamoja na wengine watano, waliambiwa na wakala wa shirika la ndege kwamba "wameondolewa kwa sababu mhudumu wa ndege wa kiume mweupe alilalamika juu ya harufu ya mwili wa abiria ambaye hakujulikana".

"Hakuna maelezo zaidi ya rangi ya ngozi yetu," wanaume hao walisema katika taarifa Jumatano, na kuongeza: "Ni wazi kuwa huu ulikuwa ubaguzi wa rangi."

Wafanyakazi wa American Airlines walijaribu kuwaweka tena watu hao kwenye safari za ndege nyingine, lakini hapakuwa na huduma nyingine kwenda New York usiku huo.

Kundi hilo wakati huo liliruhusiwa kuchukua tena viti vyao kwenye ndege yao ya awali. American Airlines ilisema katika taarifa: "Tunachukua madai yote ya ubaguzi kwa uzito mkubwa na tunataka wateja wetu wapokee huduma nzuri wanapochagua kusafiri nasi.

"Timu zetu kwa sasa zinachunguza suala hilo, kwani madai hayo hayaakisi maadili yetu ya msingi au madhumuni yetu ya kujali watu."

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo