Baraza la vita la Israel ni nini na kwanini baadhi ya wajumbe wamejiuzulu?

 

Siku ya Jumapili usiku, Baraza la Vita la Israel lilifanya mkutano kwa mara ya kwanza bila mawaziri wawili wa baraza hilo, Benny Gantz na Gadi Eisenkot, ambao walitangaza kujiuzulu kutoka serikali ya dharura mapema usiku huo.

Gantz na Eisenkot walijiunga na serikali iliyoundwa na Netanyahu Oktoba 11, kufuatia kuzuka kwa vita, na ikaitwa serikali ya dharura.

Gantz na Eisenkot awali hawakuwa sehemu ya serikali kabla ya vita dhidi ya Hamas, na kwa hivyo kujiondoa kwao kutoka serikali ya Netanyahu hakumaanishi kuanguka kwa serikali.

Lakini ndio mwisho wa kile kilichoitwa "serikali ya dharura" na serikali inarudi kama ilivyokuwa kabla ya vita.

Gantz alitoa wito kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufanya uchaguzi haraka iwezekanavyo, akisema: "Tunaondoka leo katika serikali ya dharura kwa moyo mzito, na uamuzi wa kuondoka serikalini ni ngumu na mchungu.”

Baraza la Vita la Israel ni nini?

M,

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Benjamin Netanyahu

Baraza la Vita la Israel ni chombo cha kisiasa na kiusalama chenye jukumu la kufanya maamuzi ya kisiasa wakati wa kuzuka kwa vita.

Braza la sasa liliundwa baada ya kuzuka Vita vya Gaza, kufuatia mashambulizi ya Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, linajumuisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi Yoav Galant, na Mkuu wa zamani wa Majeshi Benny Gantz.

Pia linajumuisha, kama waangalizi, generali wa jeshi, Gadi Eisenkot, na Waziri wa Masuala ya Mikakati, Ron Dermer.

Baraza la Vita halichukuliwi kuwa baraza linalotambulika kikatiba. Badala yake, baraza lililoidhinishwa kisheria kufanya maamuzi ya kijeshi ni baraza dogo la mawaziri.

Wazo la kuunda serikali ya dharura wakati wa vita lilianzia 1967, wakati mkuu wa Chama cha Herut, ambacho kwa sasa kinaitwa Chama cha Likud, Menachem Begin, alipojiunga na serikali ya Chama cha Labour iliyoongozwa na Levi Eshkol, kabla ya kuzuka vita vya Juni 1967, na serikali hiyo iliendelea katika kipindi chote cha vita.

Baraza la vita lilianzishwa wakati wa Vita vya Oktoba 1973, na wanachama walifanya maamuzi ya kijeshi bila kushauriana na serikali.

Baraza la Vita la Israel lina jukumu katika kusimamia uendeshaji wa operesheni za kijeshi huko Gaza, ndicho chombo kinachosimamia vita kwa njia ya vitendo, na Baraza dogo la Mawaziri linaidhinisha mapendekezo na maamuzi ya Baraza la Vita.

Baraza la Vita ndilo lililotangaza lengo la kuanzisha vita vinavyoendelea huko Gaza, ili kuliondoa vuguvugu la Hamas na kuwakomboa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na harakati ya Hamas.

Wajumbe wa baraza la vita ni akina nani?

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu: Mwanasiasa na mwanadiplomasia mwenye uzoefu na masuala ya kijeshi kwa takribani miongo minne. Wakati wa uongozi wake kama waziri mkuu, vita sita vimezuka kati ya Israel na Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Ulinzi Yoav Galant: Alihudumu miaka 35 katika jeshi na kushiriki katika vita vingi vya Israel, kisha aliingia kwenye uwanja wa kisiasa kufuatia kushindwa kushika nafasi ya Mkuu wa Majeshi kwa sababu alituhumiwa kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu wakati wa vita vya 2008 kwenye Ukanda wa Gaza.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Benny Gantz: Ana uzoefu wa kijeshi na kisiasa. Aliongoza vita vya Israel mwaka 2012 na 2014 kwenye Ukanda wa Gaza.

Jenerali wa Jeshi na mkuu wa zamani wa jeshi, Gadi Eisenkot na Waziri wa Masuala ya Mikakati Ron Dermer pia wapo katika baraza hilo kama waangalizi.

Chanzo cha Mvutano

jk

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Gantz (kulia) na Eisenkot (kushoto)

Mzozo ulizuka kati ya Netanyahu na Gallant kuhusu hatima ya Gaza baada ya vita, Gallant akikataa Israel kusimamia Ukanda huo.

Hayo yalijiri baada ya kauli ya Netanyahu, Mei 15 mwaka jana, alisisitiza kabla ya kuunda utawala mpya mbadala wa Hamas ni lazima kwanza Hamas iondolewe madarakani na alitaka lengo hilo lifikiwe bila visingizio.

Lakini Gallant, aliishutumu serikali kwa kutojadili pendekezo la kuunda utawala wa Palestina bila Hamas baada ya vita.

Hapo awali Netanyahu alitangaza Israel itadhibiti kikamilifu usalama katika Ukanda wa Gaza baada ya kuisambaratisha Hamas.

Kwa hivyo Netanyahu alikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa Gallant kuhusu mpango wa baada ya vita katika Ukanda wa Gaza, kwani Waziri wa Ulinzi anapinga utawala wowote wa kijeshi wa muda mrefu wa Israel huko Ukanda wa Gaza.

Gantz pia alionyesha kuunga mkono upinzani wa Gallant, akielezea katika taarifa yake kwamba Gallant "alisema ukweli," akiongeza kuwa jukumu la uongozi "ni kufanya kile ambacho ni sahihi kwa nchi, kwa gharama yoyote."

Baada ya Gantz kuunga mkono kilichosemwa na Gallant, Netanyahu alijibu na kusema hayuko tayari "kuindoa Hamastan na kuiweka Fatahestan," akimaanisha Mamlaka ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi.

Netanyahu alieleza "hakukuwa na maana kuzungumzia juu za siku za baadae baada ya vita huko Gaza kama harakati ya Hamas bado ipo hai, akisisitiza ahadi yake ya kutafuta ushindi wa kijeshi, kisiasa na kitaifa.

Galant na Gantz wanaunga mkono sera zinazoungwa mkono na jeshi na taasisi za usalama, sera zinazozingatia suala la nani atatawala Gaza baada ya vita.

Wachambuzi wa mambo wanaamini, mpasuko wa Israel unaozidi kuongezeka, unaongeza shinikizo kwa Netanyahu.

Waziri Mkuu anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa washirika wake wa mrengo mkali wa kulia, ambao wametishia kujiuzulu kutoka serikalini ikiwa ataendelea na pendekezo la kusitisha vita na kubadilishana wafungwa lililotangazwa na Rais wa Marekani Joe Biden mwezi uliopita.

Washirika hao ni Waziri wa Usalama wa Taifa Itamar Ben Gvir na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich, walisisitiza serikali haipaswi kukubali makubaliano yoyote ya amani na iendelee na vita hadi lengo kuu la kuiangamiza Hamas lifikiwe.

 

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China