HAMAS na Jihadul-Islami zakabidhi rasmi majibu yao kwa mpango wa kusimamisha vita Ghaza
Harakati kuu za Muqawama na ukombozi wa Palestina za HAMAS na Jihadul-Islami zimetoa jibu rasmi kwa pendekezo linaloungwa mkono na Marekani la kusitisha mapigano Ghaza na kubadilishana mateka kwa wafungwa kwa kuongeza baadhi ya "maoni" kuhusu mpango huo. Hayo yamethibitishwa na wapatanishi wa Qatar na Misri.
Afisa mwandamizi wa Hamas Osama Hamdan ameiambia kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen ya Lebanon kwamba harakati yao "imewasilisha baadhi ya maoni kuhusu pendekezo hilo kwa wapatanishi".
Hamdan amefafanua kuwa majibu ya Hamas yametilia mkazo msimamo kwamba makubaliano yoyote lazima yakomeshe uchokozi wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina, yahakikishe wanajeshi wa Israel wanaondoka kikamilifu Ghaza, kujengwa upya eneo hilo na kufikiwa makubaliano ya maana ya kubadilishana wafungwa.
Kwa mujibu wa duru za habari, sehemu ya maoni ya marekebisho yaliyowasilishwa katika jibu la Hamas na Jihadul-Islami kwa mpango uliopendekezwa na Marekani na kuungwa mkono na azimio la Umoja wa Mataifa inajumuisha kuondoka kikamilifu jeshi la Kizayuni katika Ukanda wote wa Ghaza, ikiwemo kivuko cha Rafah na Ukanda wa Philadelphia.
Wizara za mambo ya nje za Qatar na Misri zimeeleza katika taarifa yao ya pamoja kwamba zinachunguza jibu hilo na kwamba zitaendelea na juhudi zao za upatanishi pamoja na Marekani "hadi makubaliano yatakapofikiwa".../