Hamas yaonyesha kuridhishwa na mapendekezo ya kusitisha mapigano Gaza
Kundi la Hamas limeonyesha kuridhishwa kwa sehemu na mapendekezo ya Israeli kuelekea usitishwaji wa mapigano kama ilivyotangazwa na rais wa Marekani Joe Biden, ambaye alitoa wito wa kumalizika kwa mapigano ya karibia miezi minane sasa.
Baada ya kauli ya Hamas, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, alionekana kutupilia mbali juhudi za rais Joe Biden kuhusu upatikanaji wa amani, akisisitiza kuwa jeshi lake litaendelea na oparesheni zake za kijeshi.
Netanyahu anasema wanajeshi wake wataendelea kupigana ilikuwazuia Hamas kutawala katika ukanda wa Gaza suala ambalo anasema iwapo litafanyika litakuwa ni tishio la kijeshi.
Taarifa ya Rais Biden imekuja pia wakati huu wanajeshi wa Israeli wakiendelea kupiga hatua katikati mwa mji wa Rafah, wakizidisha makabiliano na wapiganaji wa Hamas licha ya wito wa jamii ya kimataifa kupinga oparesheni za kijeshi katika mji huo wa kusini mwa Gaza.
Akieleza namna vita hivyo vinaweza kumalizika, Rais Biden alisema mapendekezo ya Israeli yamo kwenye awamu tatu ikiwemo wanajeshi wake kujiondoa katika maeneo yote yenye idadi kubwa ya raia katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha wiki sita.
Mateka wanaozuiliwa katika ukanda wa Gaza wikiwemo wanawake, wakongwe na watu waliojeruhiwa wanatarajiwa pia kuachiwa huru, Israeli nayo ikiwaachia mamia ya wafungwa wa Palestina.
Baada ya matakwa hayo kutelezwa, maofisa wa Israeli na Palestina wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya namna ya kuafikia usitishwaji wa vita wa kudumu katika kipindi hicho cha wiki sita.
Rais Biden pia ameeleza kuwa mapigano yatakuwa yamesitishwa wakati wa mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika katika muda wa wiki sita.
Joe Biden, Rais wa Marekani alikuwa ametoa wito kwa Hamas kukubali mapendekezo ya Israeli, matamshi yaliooungwa mkono na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza David Cameron.
Soma pia