Hizbullah: Israel itapata 'mshangao mkubwa' ikianzisha vita dhidi ya Lebanon
Afisa wa ngazi za juu wa harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon amesema harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kwa hali yoyote inayoweza kutokea, na kusisitiza kwamba Israel itapata mshangao mkubwa zaidi ya huko nyuma iwapo itaamua kuanzisha vita vipya dhidi ya Lebanon.
Naibu Katibu Mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem amesema kile ambacho Hizbullah tayari imeonyesha katika kipindi cha vita vya kuunga mkono Gaza na katika kuilinda Lebanon ni sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kijeshi.
Sheikh Qassem amesisitiza kwamba Hizbullah haitaki vita lakini amesema “Ikiwa adui anataka kuanzisha vita vipya (dhidi ya Lebanon) basi Hizbullah hatutasita kujibu. Waisraeli wanafahamu ukweli huo.”
Naibu mkuu wa Hizbullah alisema kwamba maendeleo ya kistratijia yanayojitokeza yanapendelea Mhimili wa Mapambano, na adui atatambua hasara kubwa waliyoipata katika ngazi zote baada ya vita hivi.
Utawala wa Israel umekuwa ukishambulia mara kwa mara eneo la kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Katika kulipiza kisasi, Hezbollah hutekeleza mashambulizi ya makombora na maroketi karibu kila siku dhidi ya ngome za jeshi katili la Israel.
Hizbullah tayari imepigana vita mara mbili na Israel mwaka 2000 na 2006. Mapambano hayo yaliulazimisha utawala huo kurudi nyuma katika migogoro yote miwili.