India: Mahujaji 10 wa Kihindu wauawa katika shambulizi dhidi ya basi

 

Polisi wanasema dereva alipoteza udhibiti baada ya basi kumiminiwa risasi

Chanzo cha picha, ANI

Maelezo ya picha, Polisi wanasema dereva alipoteza udhibiti baada ya basi kumiminiwa risasi

Takriban watu 10 wamefariki na wengine 33 kujeruhiwa baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye silaha kushambulia basi lililokuwa limewabeba mahujaji wa Kihindu katika eneo la Jammu na Kashmir huko India, maafisa wa polisi wanasema.

Dereva alipoteza udhibiti, na kusababisha basi kutumbukia kwenye korongo katika wilaya ya Reasi ya Jammu, waliongeza.

Ingawa shughuli za uokoaji zimekamilika, jeshi la India na polsi wameanzisha operesheni ya kuwasaka wanashambuliaji hao.

Maafisa walisema Waziri Mkuu Narendra Modi amefahamishwa "hali ilivyo" na ameomba huduma bora ya matibabu itolewe kwa waliojeruhiwa.

"Wale wote waliohusika na kitendo hiki kiovu wataadhibiwa hivi karibuni," Manoj Sinha, msimamizi mkuu wa eneo hilo, aliandika kwenye X (zamani Twitter).

Maafisa wanasema basi hilo lilikuwa likielekea katika kambi ya watu mashuhuri ya Kihindu ya Mata Vaishno Devi wakati liliposhambuliwa.

Hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo lakini Mohita Sharma, mkuu wa polisi wa wilaya, aliambia shirika la habari la Reuters kwamba washukiwa "waliovamia basi" ni wanamgambo .

Eneo la Himalaya la Kashmir limekuwa likizozaniwa kati ya India na Pakistan kwa zaidi ya miongo sita.

Tangu mwaka wa 1947, majirani hao wenye silaha za nyuklia wamepigana vita viwili kwenye eneo hilo lenye Waislamu wengi, ambao wote wanadai kwa ukamilifu lakini wanadhibiti kwa sehemu.

Tangu 1989, Kashmir inayotawaliwa na India pia imeshuhudia uasi wa kutumia silaha dhidi ya utawala wa Delhi, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maidha.

Delhi inaishutumu Islamabad kwa kuwahifadhi wanamgambo na kuvuruga amani katika eneo hilo, madai ambayo Pakistan inakanusha.

Taarifa za shambulio la Jumapili ziliibuka wakati Bw Modi akila kiapo cha waziri mkuu wa India kwa muhula wa tatu mfululizo katika hafla ya kuapishwa huko Delhi.

Abiria hao bado hawajatambuliwa lakini inaaminika wanatoka jimbo la kaskazini mwa India la Uttar Pradesh, Bi Sharma aliambia gazeti moja.

Picha zilionyesha baadhi ya watu waliojeruhiwa akiwemo mwanamke mmoja wakipelekwa hospitali ya Jammu kwa matibabu.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China