Kampeni za uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wake zaanza rasmi nchini Iran
Siku ya kwanza ya kampeni za uchaguzi wa kabla ya wakati wake zimeanza leo rasmi hapa nchini Iran kwa wagombea kupewa muda sawa wa kutangaza sera zao katika kanali mbalimbali za redio na televisheni ya taifa.
Kwa mujibu wa Kanali ya Sahab, walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi huo wa 14 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Iran, Mostafa Pourmohammadi, Waziri wa zamani wa Afya, Massoud Pezeshkian na Amirhossein Ghazizadeh-Hashemi, Mkuu wa Wakfu wa Masuala ya Mashahidi na Maveterani.
Wengine waliopasishwa kugombea nafasi hiyo iliyobaki wazi baada ya kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta Mei 19 mwaka huu, ni Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), Mohammad Baqer Qalibaf, Meya wa jiji la Tehran, Alireza Zakani, na Saeed Jalili, mjumbe mkuu wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran.
Kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha Katiba ya Iran, kampeni hizo za uchaguzi wa rais zitaendelea hadi saa 24 kabla ya zoezi la upigaji kura na kwa uchaguzi huu, kampeni hizo zitamalizika saa mbili asubuhi ya siku ya Alkhamisi ya tarehe 27 Juni, 2024.
Kabla ya hapo Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran yalikuwa yametangaza orodha ya mwisho ya shakhsia waliodhinishwa kugombea uchaguzi huo wa mapema wa duru ya 14 ya rais wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mohsen Eslami, Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi ya Iran alisema shakhsia sita ndio waliodhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba la Iran lenye wanachama 12, kugombea uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Juni 28 hapa nchini.
Kuna shakhsia wengi waliojiandikisha kugombea urais huo lakini hawakupita katika mchujo. Baadhi ya shakhsia hao wakubwa waliotemwa kwenye mchujo wa Baraza la Kulinda Katiba la Iran ni pamoja na Mahmoud Ahmadinejad, rais wa zamani wa Iran, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Es’haq Jahangiri na Mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Zohreh Elahian ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kujiandikisha kugombea uchaguzi wa rais wa mwaka huu 2024.