Kiongozi wa Hizbullah aishukuru Iran kwa kuunga mkono muqawama, mataifa ya eneo
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ametoa shukurani zake za dhati kwa Iran kwa uungaji mkono wake "imara" kwa mataifa ya eneo na harakati za muqawama (mapambano ya Kiislamu) katika eneo.
Katika kikao na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani siku ya Jumanne, Sayyed Hassan Nasrallah alimshukuru Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, pamoja na serikali na taifa la Iran, kwa misimamo yao isiyoyumba ya kuunga mkono muqawama dhidi ya vikwazo na vitisho.
Pia katika kikao hicho ametuma tena salamu zake za rambirambi kutokana na kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian katika ajali ya helikopta mwezi uliopita.
Wakati wa mkutano huo, Nasrullah na Bagheri Kani wamejadili matukio ya hivi karibuni ya kisiasa na kiusalama katika eneo, hususan yale ya pande za Gaza na Lebanon.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisafiri Jumatatu nchini Lebanon, ambako amekutana na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati, Waziri wa Mambo ya Nje Abdallah Bou Habib na Spika wa Bunge Nabih Berri.
Pia amewasilisha rambirambi zake kufuatua kuaga dunia mama yake Nasrallah, Mahdiyya Safi al-Din, ambaye alifariki dunia hivi karibuni.
Ziara ya Lebanon imekuwa hatua ya kwanza kikanda ya mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ambayo pia imempeleka Syria leo Jumanne.