Mabilionea wanaomuunga mkono Trump licha ya kukutwa na hatia
Wafadhili matajiri zaidi wa chama cha Republican wanamuunga mkono Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kufuatia kesi ya kihistoria dhidi yake na kukutwa na hatia ya uhalifu.
Trump, mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa Novemba wa Ikulu ya White House, alipatikana na hatia ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha pesa zilizolipwa kwa nyota wa zamani wa filamu ya watu wazima Stormy Daniels.
Ingawa amesalia nyuma ya Joe Biden na juhudi za Democrats za kuchangisha pesa, hatia hiyo iliingiza nguvu mpya katika jitihada zake za uchaguzi - huku kampeni yake ikitangaza kwamba ilichangisha karibu $53m (£41.6m) ndani ya saa 24 tu baada ya uamuzi huo mahakama.
Bilionea wa kasino wa Israel na Marekani Miriam Adelson anatarajiwa kutangaza nyongeza ya mamilioni ya dola kwa kampeni ya Trump wiki hii.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, Bi.Adelson atatoa mchango kwa kamati ya utendaji ya kisiasa iitwayo Preserve America. Kamati za utekelezaji wa kisiasa zinaweza kutumia kiasi kisicho na kikomo cha pesa kuunga mkono wagombeaji wa nyadhifa za kuchaguliwa.
Ingawa haijafahamika ni kiasi gani anapanga kutumia, Politico na vyombo vingine vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba mchango huo unatarajiwa kuzidi mchango wa $90m kwa Preserve America wa Bi Adelson na marehemu mumewe, Sheldon, kabla ya uchaguzi wa 2020.
Wengine wana uwezekano wa kufuata mfano huo. Saa chache baada ya uamuzi huo wiki iliyopita, mabilionea kadhaa matajiri walichapisha jumbe za kumuunga mkono Trump.
Miongoni mwao alikuwa mwekezaji wa Silicon Valley David Sacks, ambaye alichapisha kwenye X, zamani Twitter, kwamba "sasa kuna suala moja tu katika uchaguzi huu: kama watu wa Marekani watasimama kwa Marekani kuwa Jamhuri ya iliyofeli".
Mnamo tarehe 6 Juni, Bw Sacks na mwekezaji mwenzake Chamath Palihapitiya, wanapanga kuandaa harambee ya kumchangishia Trump fedha huko San Francisco. Wahudhuriaji wanaripotiwa kuombwa kuchangia kiasi cha $300,000.
Mfadhili mwingine anayetarajiwa, meneja wa mfuko wa uwekezaji Bill Ackman, anatarajiwa kutoa tangazo kwenye X katika siku zijazo kuhusu kumuunga mkono Trump.
Ingawa miaka mitatu iliyopita Bw Ackman alisema kwamba Trump "anapaswa kuomba msamaha kwa Wamarekani wote" kufuatia ghasia za Bunge la Capitol la Marekani, mfadhili huyo alilegeza msimamo wake kutoa maneno ya kumuunga mkono rais huyo wa zamani mtandaoni.
Afisa mkuu Mtendaji wa Blackstone Group Steve Schwarzman - mmoja wa mabilionea mashuhuri zaidi Wall Street - tayari ametangaza kumuunga mkono Trump katika uchaguzi huo.
Kama Bw Ackman, Bw Schwarzman hapo awali alikuwa amejitenga na rais huyo wa zamani.
Lakini mwishoni mwa mwezi Mei, Bw Schwarzman alisema kuwa alishiriki "wasiwasi wa Wamarekani wengi kwamba sera zetu za kiuchumi, uhamiaji na mambo ya nje zinaipeleka nchi katika mwelekeo mbaya".
Pia alisema "kuongezeka kwa kasi kwa chuki kumenifanya kuangazia matokeo ya uchaguzi ujao kwa dharura zaidi".
Mabilionea wengine mashuhuri ambao wamemuunga mkono Trump hadi sasa ni pamoja na waanzilishi wa mfuko wa uwekezaji John Paulson na Robert Mercer, pamoja na waanzilishi wa zamani Harold Hamm na bwenyenye wa kasino Steve Wynn.
Mwekezaji bilionea Nelson Peltz - ambaye alisema baada ya ghasia za Bunge la Marekani kwamba alijuta kumpigia kura Trump mnamo 2020 - amebadilisha nia na alimkaribisha rais huyo wa zamani katika jumba lake la kifahari la Florida mnamo Machi.
Elon Musk, kwa upande mwingine, hapo awali alisema hatachangia mgombea yeyote katika kipindi hiki cha uchaguzi, ingawa ana mpango wa kuandaa hafla ya mazungumzo ya ukumbi na Trump.
Vile vile, mfadhili wa teknolojia bilionea na mfadhili mashuhuri wa chama cha Republican Peter Thiel ameripotiwa kukataa maombi ya kuchangia kampeni ya Trump na ilisemekana hakupanga michango yoyote katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Shaun Maguire, mshirika katika kampuni maarufu ya mtaji wa Sequoia, alitangaza mchango wa $300,000 kwa Trump ndani ya dakika chache za uamuzi wa wiki iliyopita, akisema kuwa kesi hiyo haikuwa ya haki.
Katika chapisho refu kwenye X, Bw Maguire alitaja sababu kadhaa za kumuunga mkono Trump, ikiwa ni pamoja na jinsi serikali ya Biden ilivyoshughulikia kujiondoa kwa Marekani kutoka Afghanistan na "udhaifu" katika Mashariki ya Kati.
Kesi mbalimbali za kisheria dhidi ya Trump, Bw Maguire aliongeza, pia zilitumika kama "uzoefu mbaya".
"Kuna uwezekano mkubwa kwamba Rais Trump atapatikana na hatia ya makosa ya jinai na kuhukumiwa kifungo," aliandika. "Kusema kweli, hiyo ndiyo sehemu ya sababu ninamuunga mkono. Ninaamini mfumo wetu wa haki umegeuzwa kuwa silaha dhidi yake."
Kufikia sasa, kampeni ya Biden kwa kiasi kikubwa imepita kampeni ya Trump hadi uchangishaji wa pesa.
Kufikia mwisho wa Aprili, kampeni hiyo ilikuwa kiasi cha kuvunja rekodi cha pesa taslimu $192m, ikilinganishwa na $93.1m za kampeni ya Trump.
Mwezi huo huo, hata hivyo, kampeni ya Trump ilichangisha $76m, na kuwapita wapinzani wao wa Democrats kwa mara ya kwanza katika kipindi hiki cha uchaguzi. Kampeni ya Biden iliongeza $51m mnamo Aprili, chini sana kutoka $90m-na zaidi iliyopatikana mwezi mmoja uliotangulia
Lakini licha ya uchangishaji wote huo, Profesa Justin Buchler, mtaalam wa fedha za kampeni kutoka Chuo Kikuu cha Case Western Reserve huko Ohio, aliambia BBC: "Pesa hazitakuwa kigezo cha kuamua mshindi'.
"Jukumu la msingi la pesa katika kampeni ni kuongeza utambuzi wa majina. Kila mtu tayari anajua Donald Trump na Joe Biden ni akina nani."
Uhakiki wa data kutoka kwa CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, umegundua kuwa uchangishaji wa fedha wa Trump huimarika katika nyakati muhimu katika vita vyake mbalimbali vya kisheria.
Kabla ya kupatikana na hatia wiki iliyopita, siku zake bora zaidi za kuchangisha pesa zilikuwa 4 Aprili mwaka jana - siku ya kushtakiwa kwake huko New York City - na vile vile Agosti 25, wakati picha yake iliyochukuliwa huko Georgia ilipotolewa.
BBC imewasiliana na kampeni za Trump na Biden ili kutoa maoni yao kuhusu uchangishaji huo.