Mawaziri wa Israel watishia kujiuzulu kutokana na mpango wa kusitisha mapigan
Mawaziri wawili wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel wametishia kujiondoa na kuuvunja muungano unaotawala iwapo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu atakubali pendekezo la kusitisha mapigano Gaza lililoanzishwa na Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Ijumaa.
Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir walisema wanapinga makubaliano yoyote kabla ya Hamas kuharibiwa.
Lakini kiongozi wa upinzani Yair Lapid ameahidi kuunga mkono serikali ikiwa Bw Netanyahu ataunga mkono mpango huo.
Waziri mkuu mwenyewe alisisitiza kuwa hakutakuwa na mapatano ya kudumu hadi uwezo wa kijeshi na uongozi wa Hamas uangamizwe na mateka wote kuachiliwa.
Pendekezo la sehemu tatu la Bw Biden litaanza kwa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa wiki sita ambapo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litajiondoa katika maeneo yenye wakazi wengi wa Gaza.
Mkataba huo hatimaye utasababisha kuachiliwa kwa mateka wote, "kusitishwa kwa uhasama" na mpango mkubwa wa ujenzi mpya wa Gaza.
Lakini katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii siku ya Jumamosi, Bw Smotrich alisema alimwambia Bw Netanyahu "hatakuwa sehemu ya serikali inayokubaliana na muhtasari uliopendekezwa na kumaliza vita bila kuharibu Hamas na kuwarudisha mateka wote".
Akirejea maneno yake, Bw Ben-Gvir alisema "mpango huo.. unamaanisha mwisho wa vita na kuachwa kwa lengo la kuangamiza Hamas. Huu ni mpango wa kizembe, ambao unajumuisha ushindi kwa ugaidi na tishio la usalama kwa Israel".
Aliapa "kuvunja serikali" badala ya kukubaliana na pendekezo hilo.
Muungano wa mrengo wa kulia wa Bw Netanyahu una idadi ndogo ya wabunge bungeni, ukiegemea makundi mengi, kikiwemo chama cha Bw Ben-Gvir cha Otzma Yehudit (Jewish Power) ambacho kinashikilia viti sita na chama cha Religious Zionism cha Bw Smotrich ambacho kinashikilia viti saba.
Lakini Yair Lapid, mmoja wa wanasiasa wa upinzani wenye ushawishi mkubwa zaidi wa Israel, alikuwa mwepesi kumuunga mkono waziri mkuu huyo. Chama chake cha Yesh Atid kinashikilia viti 24.
Alisema Bw Netanyahu "ana usalama wetu kwa mpango wa kutekwa kama Ben-Gvir na Smotrich wataiacha serikali".
Mzozo huo ulikuja huku makumi ya maelfu ya watu wakiandamana mjini Tel Aviv, wakiitaka serikali ya Israel kukubali mpango uliopendekezwa na Bw Biden. Pia walimtaka Bw Netanyahu ajiuzulu.
Mzozo ulianza kati ya waandamanaji na polisi, na baadhi ya waandamanaji waliripotiwa kukamatwa.