Moto wa kaskazini wachochea Israel kuchukua hatua kumaliza mzozo unaozidi kuongezeka na Hezbollah
Makombora ya Hezbollah yamesababisha moto wa siku kadhaa kaskazini mwa Israel, huku maeneo ya hifadhi ya msitu yakiharibiwa na watu 11 wamelazwa hospitalini kwa kuvuta moshi.
Vipande vya ardhi iliyoungua vinaanza kuonekana nusu saa kutoka kwenye mpaka wa Lebanon, moshi wa rangi ya kijivu ukitoa ramani ya njia kuelekea pande zote za milima.
Wakaazi wa eneo hilo katika jamii za kaskazini zilizoachwa kwa kiasi kikubwa na Israel, wamekuwa wakipambana na moto uliotawanyika kwa wiki kadhaa.
Mwanachama mmoja wa timu ya ulinzi wa raia alisema kumekuwa na moto mara 15-16 katika eneo hilo tangu wakati huo.
Wazima moto Jumatatu walipambana kwa saa 20 kuzima moto karibu na mji wa Kiryat Shmona.
Moto huo - ambao wasimamizi wa misitu wanasema hadi sasa umeteketeza ekari 3,500 za ardhi - unachochea madai mapya kwamba serikali ya Israel ichukue hatua kumaliza mzozo unaozidi kuongezeka na Hezbollah katika upande wake wa kaskazini.
Baraza la mawaziri la vita la Israel lilitarajiwa kukutana Jumanne jioni kujadili hali mbaya ya usalama katika mpaka wake wa kaskazini. Israel na Hezbollah zimekuwa na mapigano ya kuvuka mpaka kila siku tangu Oktoba mwaka jana na wiki za hivi karibuni zimeshuhudia kuongezeka kwa mashambulizi.
Wakaazi wa kibbutz moja walisema mashambulizi ya roketi ya Hezbollah "bila shaka" yanahusishwa na vitendo vya Israel huko Gaza, na kwamba tangu operesheni ya ardhini ya jeshi la Israel katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah kuanza, roketi tatu au nne zilikuwa zikiruka juu ya nyumba zao kila siku.
Makumi kwa maelfu ya wakaazi, waliohamishwa kutoka eneo hilo baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, bado wanasubiri kurejea makwao. Lakini siku zilizowekwa na serikali kutangaza maeneo hayo kuwa huru tena zinaendelea kusonga.
Wengi wa wakaazi hao waliokimbia makazi yao wanaona kusitishwa kwa mapigano huko Gaza kama njia muhimu ya kutuliza hali ya kaskazini.