Sheinbaum kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Mexico - kura za maoni
Mgombea aliyekuwa kifua mbele katika kinyang’anyiro cha urais Mexico Claudia Sheinbaum anatarajiwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Mexico katika ushindi wa kihistoria, kura za maoni za mwisho zinaonyesha.
Wadadisi walitabiri kuwa meya huyo wa zamani wa Mexico City mwenye umri wa miaka 61 alikuwa ameshinda 56% ya kura katika uchaguzi wa Jumapili, na kumshinda mpinzani wake mkuu, mfanyabiashara Xóchitl Gálvez.
Chama cha Bi Sheinbaum cha Morena tayari kimedai ushindi - lakini Bi Gálvez aliwataka wafuasi wake kusubiri matokeo rasmi, yanayotarajiwa kutangazwa mapema Jumatatu.
Wapiga kura pia walikuwa wakiwachagua wajumbe wote wa Bunge la Mexico na magavana katika majimbo manane, pamoja na mkuu wa serikali ya Mexico City, katika kampeni hiyo iliyokumbwa na mashambulizi makali.
Serikali inasema zaidi ya wagombea 20 wa eneo hilo wameuawa kote Mexico, ingawa tafiti za kibinafsi zinaweka jumla ya 37 waliuawa.
Watu wawili waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi mawili kwenye vituo vya kupigia kura katika jimbo la Puebla siku ya Jumapili, maafisa walisema.