Trump ataka jaji kuondoa amri dhidi ya kuzungumzia kesi ya malipo ya nyota wa filamu za watu wazima

.

Mawakili wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wamemtaka jaji anayesimamia kesi ya malipo ya fedha kwa nyota wa filamu za watu wazima mjini New York kuondoa amri aliyowekewa Trump dhidi ya kuzungumzia kesi hiyo hadi itakapokamilika.

Barua iliyotumwa kwa Jaji Juan Merchan siku ya Jumatatu inasema kwamba wasiwasi wa mahakama "hauhalalishi vizuizi vinavyoendelea" kwa haki ya uhuru wa kujieleza ya Trump.

Siku ya Alhamisi, Trump alipatikana na hatia ya makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara zinazohusisha malipo ya kumnyamazisha nyota ya ponografia ambaye anasema alifanya naye ngono.

Amri hiyo ilitolewa mnamo Machi 26, ikipiga marufuku Trump kuzungumza hadharani juu ya mashahidi, majaji, waendesha mashtaka, wafanyikazi wa mahakama na wanafamilia wao.

Mawakili wa Trump Todd Blanche na Emil Bove waliandika katika barua kwa jaji kwamba Trump anapaswa kufurahia "kampeni isiozuiliwa".

Wanasema kesi yake "imefanywa kuwa na nguvu zaidi" baada ya mpinzani wake wa kisiasa, Rais wa Marekani Joe Biden, kuzungumza hadharani kuhusu kesi hiyo.

Wanaongeza kuwa Trump kwa sasa hawezi kujitetea dhidi ya "mashambulizi ya hadharani yanayoendelea" na mashahidi wa upande wa mashtaka, kama vile wakili wake wa zamani Michael Cohen na nyota wa ponografia, Stormy Daniels.

Barua hiyo pia inataja ushiriki wa Trump katika mjadala wa kwanza wa urais dhidi ya Bw Biden, uliopangwa kufanyika tarehe 27 Juni.

Trump atahukumiwa na Jaji Merchan tarehe 11 Julai, siku nne kabla ya kutangazwa rasmi kuwa mteule wa urais wa Chama cha Republican.

Timu yake imetoa maombi mara kwa mara ya awali ya kuondoa amri hiyo, lakini hayo yamekataliwa na hakimu.

Wakati wa kesi Jaji Merchan alimtoza Trump faini ya $10,000 (£7,800) kwa kukiuka agizo hilo la kutozungumzia kesi, na kutishia kumfunga jela ikiwa ataendelea.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo