UN yathibitisha kukamatwa kwa wafanyakazi wake 11 na waasi wa Houthi nchini Yemen
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wafanyakazi wake 11 ambao wamezuiliwa na vuguvugu la Houthi nchini Yemen.
Wafanyakazi hao walichukuliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yenye migogoro, katika kile kinachoonekana kuwa msako.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric alisema chombo hicho cha dunia kinafuatilia njia zote ili kupata kuachiliwa kwao kwa usalama na bila masharti haraka iwezekanavyo.
Kundi hilo lenye silaha linajiona kama sehemu ya "mhimili wa upinzani" unaoongozwa na Iran dhidi ya Israel, Marekani na Magharibi kwa upana, na limetangaza uungaji mkono wake kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Wahouthi wamekuwa wakilenga meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya anga ya Marekani na washirika wake.
Wafanyakazi kadhaa wa mashirika mengine ya kimataifa pia walizuiliwa, ripoti zilizonukuu maafisa kutoka serikali inayotambulika kimataifa ya Yemen zilisema.
Simu na kompyuta zilinaswa wakati wa uvamizi wa nyumba na ofisi za wafanyikazi, ambao umekuja baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya Houthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu.
Kuzuiliwa huko kunaonyesha hatari zinazowakabili wafanyikazi wa misaada katika nchi ambayo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muongo mmoja vimeripotiwa kuua zaidi ya watu 150,000 na kusababisha moja ya migogoro mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Wahouthi wakikabiliwa na matatizo ya kiuchumi yanayoongezeka na mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano unaoongozwa na Marekani.
Kundi hilo lenye silaha linadhibiti mji mkuu wa Yemen, Sana'a na kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, likiendesha serikali ya ukweli ambayo inakusanya kodi na kuchapisha pesa.
Serikali inayotambulika kimataifa ya Yemen iko katika bandari ya kusini ya Aden.