Wajue wagombea wa urais Marekani waliogombea wakiwa gerezani

 

Katika siku ambayo haijawahi kushuhudiwa katika siasa za Marekani, Donald Trump amekuwa rais wa kwanza mstaafu wa Marekani kupatikana na hatia ya uhalifu.

Wataalamu wengi wanakubaliana kuwa huenda asitumikie kifungo kwa makosa 34 ambayo amepatikana na hatia katika hukumu itakayo tolewa siku ya Alhamisi katika chumba cha mahakama cha Manhattan.

Bado ana uwezo wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo - mchakato ambao pengine utaendelea hadi uchaguzi wa Novemba au zaidi.

Hata kama hukumu itathibitishwa, huenda akapigwa faini, au akawekwa katika kipindi cha uangalizi. Lakini hata ikiwa atakwenda jela - Trump anaweza kuendelea kuwa mgombea na uwezekano wa kuwa rais wa Marekani akiwa jela.

Matakwa ya Kuwa Rais

Matakwa ya kisheria kwa wagombea urais hayajabadilika tangu 1789, mwaka ambapo George Washington akiwa rais wa kwanza wa Marekani.

"Sifa ya kuwa mgombea ni lazima awe umezaliwa Marekani au katika maeneo yake. Na anapaswa kuwa na umri fulani ambao ni kuanzia umri wa miaka 35,” anasema Prof Iwan Morgan, profesa mstaafu wa historia ya Marekani katika Chuo Kikuu cha London.

Mgombea pia awe amekaa Marekani kwa miaka 14 – takwa lililowekwa baada ya Vita vya wenyewe kwa wenyewe ili kuwazuia watu ambao waliasi dhidi ya Marekani," anasema Prof Morgan.

Lakini hakuna marufuku kwa wahalifu waliopatikana na hatia kugombea Ikulu ya White House. Na kuna sababu ya kihistoria katika hilo.

"Marekani ilizaliwa kutokana na mapinduzi, na kulikuwa na uwezekano kwamba mtu ambaye aliwekwa gerezani kwa kupinga ufalme - Marekani ilipokuwa koloni la Uingereza - angeweza kuondolewa kuwania urais."

“Hakuna hata mmoja miongoni mwa waanzilishi wa mkataba ambao uliunda katiba ya Marekani mwaka 1787 - waliofungwa na Waingereza, lakini wengine walikaribia kufungwa," anasema Prof Morgan.

"Kama mapinduzi yasingefaulu, wangekuwa na hatia ya uhaini dhidi ya ufalme, na wangekuwa wahalifu."

Hii ndiyo sababu waandishi wa katiba hawakutaka kuweka vikwazo juu ya nani anaweza kuwa rais. Na sera imesababisha wagombea watatu kufanya kampeni za urais wakiwa ndani ya gereza.

Eugene V Debs

Eugene V Debs in 1912

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Eugene V Debs's aligombea uraisi 1912 na 1920 kipindi cha mafanikio makubwa kwa ujamaa Marekani

"Mgombea aliyegombea nafasi ya urais akiwa katika gereza la serikali alikuwa Eugene Debs mwaka 1920," anasema Prof Morgan.

Debs alikuwa gerezani kwa mara ya kwanza mwaka 1894. Kama afisa wa chama cha wafanyakazi aliongoza upinzani dhidi ya kampuni ya treni, alipatikana na hatia ya kuzuia barua za posta.

Jeshi lilivunja mgomo huo na Debs akaenda jela kwa miezi sita.

“Mapema katika Karne ya 20, akawa mwanachama wa Chama cha Kisoshalisti cha Marekani. Aligombea urais 1904, 1908, 1912 na 1920,” Prof Morgan anaeleza (Debs pia aligombea kwa tiketi ya Social Democratic Party mwaka 1900).

"Mwaka 1912, katika kinyang'anyiro cha wagombea wa nne kilichohusisha Democrat, Woodrow Wilson, Republican, William Howard Taft, mgombea wa Progressive na Rais wa zamani wa Republican Theodore Roosevelt, na Debs ambaye alifanya vyema sana."

Alipata karibu kura milioni moja, 6% ya kura zote, "asilimia kubwa zaidi kuwahi kushinda mgombea wa Chama cha Kisoshalisti huko Marekani."

Lakini wakati wa vita vya Kwanza vya Dunia. Debs alipinga vita na kuwashawishi Wamarekani wasishiriki katika vita.

"Mapema wakati wa msimu wa vuli wa 1918 - vita vilikuwa karibu kwisha wakati huo - alitoa hotuba huko Canton, Ohio, aliwahimiza Wamarekani kupinga kuandikishwa jeshini," anasema Prof Morgan.

Debs alishtakiwa kwa uchochezi na kupelekwa gerezani katika Gereza la Shirikisho la Atlanta Aprili 1919. Bado alikuwa katika gereza hilo wakati wa uchaguzi mwaka uliofuata, na Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilimteua kuwa mgombea wao.

Debs alishinda kura nyingi zaidi kuliko alizopata mwaka 1912 (kura 914,191 mwaka 1920 na 901,551 mwaka 1912). Lakini wakati huu alipata 3% tu ya kura zote, baada ya wanawake kuruhusiwa kupiga kura.

Aliachiliwa baada ya kutumikia karibu miaka mitatu gerezani, lakini afya yake haikupata nafuu na alikufa mwaka 1926.

Baada ya Debs, vyama vya kisoshalisti nchini Marekani havikufanya vyema tena kwenye uchaguzi wa Marekani.

Lyndon LaRouche

Right-wing politician Lyndon H LaRouche speaking at a press conference in 1987

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, LaRouche alifanya harakati za kisiasa na mitazamo ya ajabu

Mgombea urais ambaye alifanya kampeni akiwa jela alikuwa Lyndon LaRouche.

"Wakati mwingine alifanya kampeni kama mdemo-Democrat, lakini mara nyingi mgombeaji mdogo, na jina lake lilikuwa katika kila uchaguzi, kuanzia 1976 hadi 2008," anasema Prof Morgan.

LaRouche alianza kujihusisha na siasa za mrengo wa kushoto katika miaka ya 1940, lakini kufikia miaka ya 1970 siasa zake zilikuwa zimehamia mrengo wa kulia.

"Watu wa Republican na Democratic walimjua kuwa ni kituko. Alikuwa na mawazo ya ajabu. Aliamini kwamba Malkia Elizabeth alikuwa anataka kumdhuru,” anasema Prof Morgan.

LaRouche aliendelea kuunda vuguvugu la kisiasa na mchanganyiko wa mitazamo yake ya ajabu kuhusu ulimwengu. Kama vile kodi ndogo na kuhakikisha kuwa serikali haipelelezi raia wake yenyewe. Hajawahi kuwa na zaidi ya watu 2,000, kulingana na Prof Morgan.

Lakini alikuwa akiwaunga mkono baadhi ya wagombea wa Democratic. Alitumia fedha kufadhili wagombea aliowaidhinisha katika chaguzi za mitaa, majimbo na bunge - ingawa mafanikio yalikuwa madogo sana.

Alifungwa jela kwa ulaghai kwa kutumia barua ya posta 1989 na akahukumiwa miaka 15.

"Ulipofika uchaguzi 1992, LaRouche aligombea," anasema Prof Morgan, "alikuwa katika kura katika majimbo machache, na kura zake nyingi ni 27,000, sawa na 0.1% ya jumla ya kura.”

Adhabu ya LaRouche ilibadilishwa na akaondoka gerezani mwaka 1994. Aliendelea kuwania urais mwaka 1996, 2000, 2004 na 2008.

“Licha ya uwezo wake wa kuchangisha pesa na kuendelea kufanya kampeni, LaRouche hakuwahi kuvutia sana,” anasema Prof Morgan.

LaRouche alifariki 2019.

Joseph Smith

Murder of Joseph and Hyrum Smith, 1844 (c1880). The Mormon Church (Church of Jesus Christ of Latter-day Saints) was founded by Joseph Smith in 1830

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwasisi wa Mormon, Joseph Smith alipigwa risasi wakati akipiga kampeni akiwa gerezani 1844

Joseph Smith alianzisha dini ya Mormonism mwaka 1830. Dini inayomtambua Yesu lakini ina tofauti kubwa na makanisa ya Kikatoliki, Kiprotestanti na Othodoksi,. Alianzisha pia mitala.

"Haikupendwa sana na wasiokuwa wafuasi wake," anasema Prof Morgan. "Ilionekana kama tishio kwa maadili ya Marekani. Ndoa ya wake wengi ilionekana kama uhalifu mbaya, Smith alidaiwa kuwa na wake 20."

Smith alikuwa anatokea Massachusetts, lakini safari zake za kutafuta sehemu salama kwa wafuasi wake ziliwapeleka magharibi hadi Illinois.

Huko Wamormoni walijenga mji wao wenyewe mwanzoni mwa miaka ya 1840, Nauvoo kwenye ukingo wa mto wa Mississippi, wakitarajia kuishi na kuabudu kwa amani.

Smith alipigiwa kura kuwa meya na kuunda wanamgambo wa Mormon.

“Lakini tatizo likawa Smith alikuwa mhusika wa mgawanyiko ndani ya Umormoni. Shughuli zake za mitala zilileta uadui miongoni mwa Wamormoni ambao, yaonekana wake zao alikuwa akiwaiba.”

Smith aliamuru wanamgambo wake kuharibu ofisi za gazeti linalompiga Smith, tukio ambalo hatimaye lilimtia gerezani huko Carthage, Illinois.

Alishindana kama mgombea wa Chama cha Reform Party katika uchaguzi wa rais wa 1844. Chama chake chenye misingi ya Mormon kilitarajia kushika hatamu, na hivyo kukuza mawazo yao ya mitala na maoni ya Smith mwenyewe kwamba kila mtu kimsingi ni Mungu.

Lakini imani ya chama hicho katika ukombozi dhidi ya utumwa kiliwaletea maadui zaidi.

“Kukomesha utumwa ni jambo ambalo halikupendwa na watu wa Kaskazini wakati huo; hata wale wasiokuwa Wamormoni ambalo walipinga utumwa walikuwa wakifanya harakati ya hatari,” anasema Prof Morgan.

Umati wa watu ulikusanyika nje ya gereza huko Carthage, na yeye na mfungwa mwingine walipigwa risasi na kufa katika jengo walimokuwa wakitafuta hifadhi.

"Kikosi cha kufyatua risasi kilipangwa ili kuupiga risasi mwili wake mara nyingi zaidi," anaongeza Prof Morgan.

Chama cha Reform hakikuendelea kusimamisha mgombea katika uchaguzi wa 1844.

Kwa hivyo kumekuwa na wagombea watatu wa urais ambao wamewania wadhifa wa urais wakiwa gerezani na kunaweza kuwa na wa nne ikiwa Joseph Maldonado-Passage atagombea Novemba.

Anajulikana pia kama Joe Exotic, nyota makala ya 2020 ya Netflix, Tiger King ametangaza kugombea urais.

Kwa sasa anatumikia kifungo cha zaidi ya miaka 20 kwa mashtaka yanayohusiana na ukatili wa wanyama na njama ya kumuua mmiliki wa bustani ya wanyama.

Hata kama Trump ataepuka kifungo, kwa maneno ya mwandishi wa BBC, John Sudworth, taifa lililogawanyika litakuwa na mhalifu aliyepatikana na hatia kama mgombeaji.

 

 

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo