Wanajeshi wa Korea Kusini wafyatua risasi za onyo baada ya wanajeshi wa Kaskazini kuvuka mpaka

.

Wanajeshi wa Korea Kusini walifyatua risasi za onyo baada ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kuvuka mpaka kimakosa, jeshi la Seoul lilisema Jumanne.

Tukio hilo lililotokea katika eneo lisilo la kijeshi (DMZ) siku ya Jumapili linajiri huku mvutano ukiendelea kuongezeka kati ya mataifa hayo ya Korea.

Kundi dogo la wanajeshi wa Korea Kaskazini lililokuwa limebeba vifaa vya shambani ikiwemo shoka liliingia Korea Kusini saa 12:30 kwa saa za huko (05:30 GMT), jeshi la Seoul liliripoti.

Walikuwa miongoni mwa watu 20 waliokuwa katika eneo la mpaka wakati huo.

Walirudi nyuma mara tu baada ya Wakorea Kusini kufyatua risasi za kutoa onyo.

Katika wiki za hivi karibuni, Kaskazini imepeperusha mamia ya puto zilizojaa taka hadi miji ya mpakani Kusini.

Seoul imejibu kwa kutangaza propaganda na muziki wa K-pop hadi Kaskazini kwa kutumia vipaza sauti.

Wanaharakati pia wamerusha puto za propaganda kuelekea Kaskazini.

Hakukuwa na harakati mashuhuri kutoka Kaskazini mwa DMZ baada ya wanajeshi wake kurudi Jumapili, jeshi la Seoul lilisema.

“Ndani ya [eneo la mpaka] mimea imeota, na alama za mpaka zimefichwa. Hakuna njia, na walikuwa wakipita kwenye miti iliokuwa," ilisema.

Siku ya Jumatatu, dadake kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Kim Yo Jong, alitishia Kusini kwa "makabiliano mapya" ikiwa itaendelea matangazo ya vipaza sauti na iwapo haitawazuia wanaharakati wake kutuma puto.

Desemba mwaka jana, Bw Kim alisitisha juhudi zote za kuungana kwa amani na Kusini, akiishutumu Seoul kwa "uadui" kuelekea Kaskazini.

Tangu wakati huo, Kaskazini ilibomoa mfano wa mnara wa kuunganisha huko Pyongyang na kumaliza mawasiliano yote na Kusini.

Mapema mwezi huu, Korea Kusini ilisitisha kile kilichosalia cha makubaliano yake ya kijeshi ya 2018 na Kaskazini, ambayo yatairuhusu kuanza tena mazoezi na shughuli za propaganda kama vile matangazo ya vipaza sauti.

Korea Kusini ilikuwa imesitisha kwa kiasi makubaliano hayo Novemba mwaka jana, kufuatia Korea Kaskazini kurusha satelaiti ya kijasusi.

Katika miezi ya hivi karibuni, Seoul iligundua wanajeshi wa Korea Kaskazini walikuwa wakitega mabomu ya ardhini kwenye mpaka na kukata reli kuelekea Kusini. Wanajeshi wa Korea Kaskazini pia walionekana wakiweka vituo vya ulinzi ndani ya DMZ.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo