Watu wenye silaha Nigeria wamewauwa watu 25 katika uvamizi wa kijiji - Maafisa
Takriban watu 25 wameuawa na wengine kutekwa nyara na watu wenye silaha katika jimbo la Katsina kaskazini magharibi mwa Nigeria, mamlaka zimesema.
Makumi ya watu waliokuwa na bunduki wakiwa na pikipiki walivamia eneo la Yargoje huko Kankara Jumapili jioni, kamishna wa masuala ya usalama wa serikali, Nasiru Babangida Mu'azu, aliambia BBC Hausa.
Mashambulizi ya magenge yenye silaha - yanayojulikana kama majambazi - kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria yamekuwa ya kawaida, na mamlaka inaonekana kukosa uwezo wa kuyazuia, licha ya madai ya serikali na vikosi vya usalama kwamba wanafanya kazi kumaliza ukosefu wa usalama ulioenea.
Wakazi waliambia BBC kwamba makumi ya watu waliokuwa na bunduki wakiwa kwenye pikipiki waliingia katika jamii, wakifyatua risasi kiholela na kupora maduka kabla ya kuwateka nyara idadi isiyojulikana ya wanakijiji."
Watu waliouawa na majambazi ni zaidi ya 50, kwa sababu baadhi ya maiti bado zinatolewa porini," alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
"Waliwaua watoto, wanawake na wanaume, na kuteka nyara idadi kubwa ya watu. Waliwajeruhi zaidi ya wakazi 30 ambao kwa sasa wanapokea matibabu katika hospitali kuu.
"Mkazi mwingine, Abdullahi Yunusa Kankara, aliiambia Reuters kwamba aliponea chupuchupu mashambulizi hayo, ambayo alisema yaliendelea hadi saa za alfajiri ya Jumatatu."Mji wetu umegeuka kuwa eneo la kifo. Takriban kila nyumba kijijini imeangukiwa na shambulio hili. Maiti zaidi zilipatikana [Jumatatu] asubuhi," alisema.
Wakaazi walionusurika wanajaribu kubaini ni watu wangapi wametekwa nyara.Mnamo Desemba 2020, zaidi ya wanafunzi 300 walitekwa nyara kutoka shule ya sekondari ya wavulana ya bweni nje kidogo ya Kankara na genge la watu wenye silaha waliokuwa wakiendesha pikipiki.
Baadaye waliachiliwa, wiki moja baada ya serikali ya jimbo la Katsina kuthibitisha kuwa walikuwa kwenye mazungumzo na watekaji nyara.
Mwezi Machi mwaka huu, makumi ya abiria walitekwa nyara katika shambulio la mchana pia katika eneo hilo hilo la Katsina, jimbo ambalo rais wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari anatokea.