Yemen yalenga kwa makombora meli kubwa ya kivita ya Marekani, USS Eisenhower, katika Bahari ya Sham
Msemaji wa jeshi la Yemen amesema wanajeshi wa nchi hiyo wameilenga meli kubwa ya kivita ya Marekani yenywe uwezo wa kubeba ndege, USS Dwight D. Eisenhower, katika Bahari ya Sham ikiwa ni katika kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Brigedia Jenerali Yahya Saree msemaji wa Majeshi ya Yemen alitangaza Ijumaa kupitia televisheni kwamba: "Vikosi vya makombora na wanamaji vya Wanajeshi wa Yemen vimefanya operesheni ya pamoja ya kijeshi iliyolenga meli ya kivita ya Marekani yenye kusheheni ndege, USS Eisenhower katika Bahari ya Sham."
Ameongeza kuwa: "Alhamdulillah, operesheni hiyo ilifanywa kwa makombora kadhaa ya balestiki, ambayo yalilenga shabaha kwa usahihi."
Jeneral Saree amesema hili lilikuwa jibu kwa mashambulizi ya angani ya Marekani na Uingereza katika maeneo kadhaa katika nchi hiyo ya Kiarabu, ambayo alisema ililenga raia katika "ukiukaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa na uhalifu kamili wa kivita."
Juzi ndege za kivita za Marekani na Uingereza zilishambulia mji mkuu wa Yemen Sana’a pamoja na mikoa ya Hudaydah na Taiz.
Jeshi la Yemen limefanya mashambulizi mengi yanayoiunga mkono Palestina tangu Oktoba 7, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Siku ya Ijumaa pia, mitaa ya Sana'a, mji mkuu wa Yemen, ilijaa makumi ya maelfu ya watu waliokuwa wakionyesha mshikamano na kadhia ya Palestina hasa kutetea Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Washiriki walipongeza hatua za jeshi la Yemen dhidi ya meli za kibiashara na kijeshi zinazohusishwa na Israel, Marekani na Uingereza, hasa mashambulizi ya karibuni vikosi vya Yemen dhidi ya meli ya kivita yenye kusheheni ndege ya USS Dwight D. Eisenhower.