Zelensky anaonya Trump akishinda urais ataachana na Ukraine - The Guardian
Gazeti la The Guardian limechapisha mahojiano ya kipekee iliyofanya na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambapo anaonya dhidi ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani na kutupilia mbali uungaji mkono wa kijeshi kwa Ukraine.
Trump aliahidi mwaka jana kwamba ikiwa atamshinda Joe Biden, angekatiza msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kumaliza vita ndani ya saa 24.
Wale walio karibu na Trump pia walidokeza mpango anaopendekeza kupeana mikoa ya mashariki ya Ukraine kwa Urusi, pamoja na Rasi ya Crimea, kumaliza mapigano.
Lakini Rais Zelensky alisisitiza kuwa nchi yake haitakubali mpango huo, wala haiko chini ya shinikizo la Urusi ambayo inajaribu kuilazimisha kuachana na wazo la kujumuika na Ulaya na kujiunga na NATO katika siku zijazo.
Rais wa Ukraine alikiri kwamba kurejea kwa Trump katika Ikulu ya White House kunaweza kuhusisha kukatisha msaada wa kijeshi na kifedha kwa nchi yake, na kwamba Ukraine haiwezi kukabiliana na jeshi la Urusi lenye uwezo mkubwa bila silaha.
Alisema jambo hilo haliwezekani kutendeka, lakini likitokea athari zake zitakuwa hatari kwa msimamo wa Marekani katika ngazi ya kimataifa, na kwa sifa ya Trump binafsi, kwani atatajwa kuwa rais aliyeshindwa na ambaye amepunguza makali ya msimamo wa Marekani.