Mapacha waliozaliwa tu wauawa baba yao akiwa ameenda kuwasajili huko Gaza

 

Mapacha waliozaliwa tu wauawa baba yao akiwa ameenda kuwasajili huko Gaza

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mapacha waliozaliwa tu wameuawa katika shambulizi la anga la Israeli huko Gaza wakati baba yao alipokuwa kwenye ofisi ya serikali ya mtaa kuandikisha kuzaliwa kwao.

Asser, mvulana, na Ayssel, msichana, walikuwa na umri wa siku nne tu baba yao Mohammed Abu al-Qumsan alipokwenda kuchukua vyeti vyao vya kuzaliwa.

Akiwa bado yuko huko, majirani zake walimpigia simu kumwambia kuwa nyumba yao huko Deir al Balah imerushiwa bomu.

Shambulizi hilo pia lilimuua mkewe na bibi ya mapacha hao.

"Sijui ni nini kilitokea," alisema. "Nimeambiwa ni kombora ambalo lilishambulia nyumba." "Sikuwa na wakati hata wa kuwasherehekea," aliongeza.

Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas inasema watoto 115 wamezaliwa tu na kisha kuuawa wakati wa vita.

Kulingana na shirika la habari la AP, familia hiyo ilifuata amri ya kuhama mji wa Gaza katika wiki za mwanzo za vita vya Israeli na kutafuta hifadhi katikati mwa ukanda huo, kama jeshi la Israeli lilivyoagiza.

BBC imelitaka jeshi la Israeli kutoa maoni yake kuhusu shambulizi hilo, na inasubiri majibu.

Israeli inasema inajaribu kuepuka kuwadhuru raia na inalaumu Hamas kwa vifo vyao, kwa madai kuwa inaendesha shughuli zake katika maeneo yenye makazi ya watu wengi, ikiwa ni pamoja na kutumia majengo ya kiraia kama makazi.

Lakini ni mara chache sana maofisa hutoa maoni juu ya mashambulizi yanayofanywa moja moja.

Makaazi kadhaa ya aina hiyo huko Gaza yameshambuliwa katika wiki chache zilizopita.

Siku ya Jumamosi, shambulizi la anga la Israeli dhidi ya jengo la shule linalohifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao katika mji wa Gaza liliua zaidi ya watu 70, mkurugenzi wa hospitali aliambia BBC.

Msemaji wa jeshi la Israeli alisema shule hiyo "inatumika kama kituo cha kijeshi cha Hamas na wanajihadi wa Kiislamu", jambo ambalo Hamas ilikanusha.

Israeli ilipinga idadi ya waliofariki iliyotolewa, lakini BBC haikuweza kuthibitisha takwimu hizo kutoka pande zote mbili.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Vita vya Urusi na Ukraine: Matukio matano muhimu ya faida na hasara kwa Putin 2024