Warusi wakimbia eneo la mpakani kufuatia madai ya uvamizi wa Ukraine

 

Warusi wakimbia eneo la mpakani kufuatia madai ya uvamizi wa Ukraine

xx

Chanzo cha picha, Reuters

Rais Vladimir Putin ameishutumu Ukraine kwa kuanzisha "uchokozi", baada ya maafisa wa ulinzi kusema takriban wanajeshi 300 wa Ukraine walivuka eneo la Kursk nchini Urusi siku ya Jumanne

Mapigano yanaripotiwa kuendelea katika eneo hilo, baada ya Moscow kusema wanajeshi wa Ukraine waliokuwa na vifaru 11 na zaidi ya magari 20 ya kivita, walivuka mpaka karibu na mji wa Sudzha, kilomita 10 kutoka mstari wa mbele.

Maelfu ya watu wametoroka kutoroka makwao katika eneo hilo. Maafisa wa Ukraine bado hawajatoa maoni yao kuhusu madai hayo ya Urusi.

Akizungumza kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama mjini Moscow, Bw Putin alishutumu vikosi vya Ukraine kwa "kufyatua risasi kiholela" katika majengo na makazi ya raia.

Mapigano yameripotiwa kutokea katika vijiji mbalimbali vya eneo la Urusi siku ya Jumanne. Ilifuatiwa na mashambulizi ya anga ya Ukraine ambayo yaliwaua raia watatu na kuendelea hadi usiku, mamlaka ya Urusi ilisema.

Watu 24, wakiwemo watoto sita, wamejeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya Ukraine katika eneo la mpakani, Moscow ilisema.

Siku ya Jumatano, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilidai kuwa ilizuia Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine "kuingia ndani ya ardhi ya Urusi" katika mkoa wa Kursk na kusema kuwa iliharibu ndege kadhaa zisizo na rubani za Ukraine usiku kucha.

Lakini, ishara za tahadhari za anga ziliendelea kutolewa huko Kursk, ambapo viongozi wa eneo hilo waliwataka wakazi kupunguza shughuli zao na hafla zote za umma ziliahirishwa.