Lebanon inasema watu 60 wameuawa katika shambulio la Israel kwenye bonde la mashariki

 

Lebanon inasema watu 60 wameuawa katika shambulio la Israel kwenye bonde la mashariki

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Takriban watu 60 wameuawa katika mashambulizi ya Israel kwenye Bonde la Bekaa Mashariki mwa Lebanon, wizara ya afya ya Lebanon imesema.

Watoto wawili walikuwa miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo ambalo lililenga maeneo 16 katika eneo la Baalbek, maafisa walisema.

Wizara hiyo ilisema watu 58 walijeruhiwa, na kuongeza kwamba juhudi za uokoaji bado zinaendelea katika bonde hilo, ambalo ni ngome ya Hezbollah.

Jeshi la Israel bado halijatoa tamko lolote.

Israel imefanya maelfu ya mashambulizi ya angani kote Lebanon katika muda wa wiki tano zilizopita, ikilenga kile inachosema ni maafisa wa Hezbollah, miundombinu na silaha.

Gavana wa Baalbek Bachie Khodr aliyataja mashambulizi hayo kuwa ya "mabaya zaidi" katika eneo hilo tangu Israel ilipozidisha mzozo dhidi ya Hezbollah mwezi uliopita.

Video ambayo haijathibitishwa iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha uharibifu wa majengo na misitu ikiteketea huku waokoaji wakiwatafuta waliojeruhiwa.

Katika mji wa Boudai, video kwenye mitandao ya kijamii zilionekana kuonyesha wakazi wakiomba vifaa vizito kutumwa kusaidia kuokoa watu wanaoaminika kuwa wamenaswa.

Mkuu wa mkoa wa kikosi cha ulinzi wa raia wa Baalbek aliiambia BBC kwamba mashambulizi ya anga yalikuwa kama "mduara wa moto".