Mithili ya tsunami': Wahispania wasimulia athari ya mafuriko mabaya
Mithili ya tsunami': Wahispania wasimulia athari ya mafuriko mabaya
"Maji yalipoanza kupanda, yalikuja kama wimbi," Guillermo Serrano Pérez alisema. "Ilikuwa kama tsunami." Kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 kutoka Paiporta, karibu na Valencia, ni mmoja wa maelfu ya watu waliokumbana na mafuriko ya Jumanne usiku ambayo yalikumba eneo hilo na kuua takriban watu 95.
Alikuwa akiendesha gari kwenye barabara hiyo na wazazi wake Jumanne jioni wakati maji yalipoingia ndani.
Walinusurika kwa kupanda daraja na kuliacha gari lao kutokana na nguvu ya maji ya mafuriko.
Mvua kubwa ilikuwa inanyesha eneo hilo kwa saa nyingi, wengi, kama vile Guillermo Serrano Pérez na familia yake, walipatwa na mafuriko bila kutarajia.
Hata hivyo dalili zilikuwepo.
Siku ya Jumanne asubuhi yapata saa 07:00 (06:00 GMT), wakala wa hali ya hewa wa Uhispania Aemet alionya kuwa mvua kubwa ilikuwa inatabiriwa katika eneo la Valencia.
"Kuwa mwangalifu sana! Hatari imekithiri! Usisafiri isipokuwa unalazika kufanya hivyo," ilisema kwenye X, kabla ya kutoa "tahadhari ya hali ya juu zaidi".
Siku nzima, tahadhari zaidi zilitolewa, zikiwaonya viongozi wa eneo hilo kuzuia watu kukaribia kingo za mito. Kufikia 15:20, kituo cha uratibu wa dharura za eneo kilikuwa tayari kikichapisha picha za mitaa iliyojaa mafuriko katika manispaa ya La Fuente na Utiel, magharibi mwa Valencia.
Saa chache baadaye, ilisema mito kadhaa katika eneo hilo ilikuwa ikifurika na kuwataka watu kuondoka kwenye kingo. Lakini katika sehemu nyingi, tayari tahadhari ilikuwa imechelewa.
Makumi ya watu bado hawajulikani walipo katika eneo lote, huku wale walionusurika wakielezea kutokuwa na la kufanya baada ya uharibifu wa kutisha.
"Tuliona magari mawili yakisombwa na mkondo wa maji na hatujui kama kulikuwa na watu ndani," mwanaume mmoja aliiambia Las Provincias. "Hatujawahi kuona kitu kama hicho."