Mshindi wa taji la Urembo nchini Rwanda akamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa
Mshindi wa taji la Urembo nchini Rwanda akamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa
Polisi nchini Rwanda wamemkamata mshindi wa taji la taifa la urembo kwa "kurudia" "kuendesha gari akiwa amekunywa pombe kupita kiasi" na kusababisha uharibifu wa miundombinu.
Divine Muheto hana leseni ya kuendesha gari na alitoroka eneo la ajali baada ya kugonga miundombinu, polisi walisema katika taarifa.
Bi Muheto hajajibu hadharani madai hayo. Bi Muheto, 21, alipata umaarufu aliposhinda shindano la urembo la Miss Rwanda mnamo 2022, kabla ya serikali kusitisha shindano hilo baada ya tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya waandaaji.
Polisi wametangaza kukamatwa kwake leo, siku chache baada ya tetesi kuwa mrembo huyo alihusika katika ajali ya barabarani na baadaye kukamatwa.
Adhabu ya kuendesha ukiwa umekunywa ni faini ya faranga 150,000 za Rwanda (dola 110), na siku tano rumande.
Katika miaka ya hivi karibuni maelfu ya watu walikamatwa kwa kosa hili huku polisi wakitekeleza sheria hii. Mnamo 2022 mbunge alijiuzulu na kuomba msamaha kwa kuendesha gari akiwa amelewa.
Utekelezaji mkali wa sheria za trafiki umepunguza kwa kiasi kikubwa ajali mbaya za barabarani nchini Rwanda, serikali imesema.
Katika taarifa yake, polisi walisema kuwa kesi ya Bi Muheto ilifikishwa katika ofisi ya mashtaka.