Ndege zisizo na rubani za Urusi zinaua raia, ushahidi unaonyesha
Ndege zisizo na rubani za Urusi zinaua raia, ushahidi unaonyesha
Kabla ya saa sita, siku moja Serhiy Dobrovolsky, mfanyabiashara wa vifaa vya nyumbani, alikuwa akirejea huko Kherson kusini mwa Ukraine.
Alipoingia ndani ya eneo lake, akawasha sigara na kuanza kuzungumza na jirani yake wa karibu.
Ghafla, walisikia sauti ya ndege isiyo na rubani nje.
Angela, mke wa Serhiy wa miaka 32, anasema alimuona mumewe akikimbia na kujificha huku ndege isiyo na rubani ikidondosha guruneti kumlenga.
"Alifariki kabla ya gari la wagonjwa kufika. Niliambiwa alikuwa na bahati mbaya kwa sababu kipande cha guruneti kilimchoma moyoni," anasema, huku akibubujikwa na machozi.
Serhiy ni mmoja wa raia 30 waliouawa katika mashambulizi ya ghafla ya ndege zisizo na rubani za Urusi huko Kherson tangu Julai 1, utawala wa kijeshi wa jiji hilo uliambia BBC.
Wamerekodi zaidi ya mashambulizi 5,000 ya ndege zisizo na rubani katika kipindi hicho, huku zaidi ya raia 400 wakijeruhiwa.
Lakini BBC imesikia ushuhuda wa mashahidi na kuona ushahidi wa kuaminika kwamba Urusi inatumia ndege zisizo na rubani pia dhidi ya raia katika mji wa Kherson ulio mstari wa mbele.
"Wanaweza kuona ni nani wanamuua," anasema Angela. "Hivi ndivyo wanavyotaka kupigana, kwa kuwalipua tu watu wanaotembea mitaani?"
Iwapo Urusi itapatikana kuwa inalenga raia kimakusudi, itakuwa ni uhalifu wa kivita.
Jeshi la Urusi halikujibu maswali ya BBC kuhusu madai hayo.