'Tutaishi vipi bila chakula' – Raia wa Gaza wahofia ukosefu wa msaada baada ya Unrwa kupigwa marufuku

 

'Tutaishi vipi bila chakula' – Raia wa Gaza wahofia ukosefu wa msaada baada ya Unrwa kupigwa marufuku

.

Chanzo cha picha, Getty Images

BBC Arabic imezungumza na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kuhusu hatua ya kupiga marufuku Unrwa.

Om Yousef

"Uamuzi wa kuzuia Unrwa kufanya kazi huko Gaza ni mbaya kwa sababu tunapata chakula kupitia wao na watoto wetu wanasomeshwa katika shule zao.

"Elimu ni jambo muhimu zaidi. Natumai uamuzi huu hautatekelezwa kwa sababu sio sahihi."

Om Sohay

"Ni uamuzi mbaya. Kwa sababu hii, hatutapata unga na mafuta.

"Hii ni ngumu sana. Tutaishi vipi bila unga, kitu pekee ambacho kinapatikana hapa nchini ni unga na bei ya mfuko mmoja ni shekeli 200 ($54) na hatuwezi kumudu, na chupa moja ya mafuta inauzwa shekeli 35 ($9).

"Kinachoendelea ni kibaya. Hatuna chochote katika nchi hii isipokuwa unga kutoka Unrwa. Tunatumai uamuzi huu utasitishwa na kufutwa kwa sababu hii ni ngumu sana."

Mohamed

"Mimi ni Mohamed niliyefukuzwa Khan Younis, walisema watasimamisha Unrwa shirika linaloleta unga, mafuta na sukari na vitu muhimu.

"Likipigwa marufuku hatutapata unga na pia wataacha kusomesha watoto.

"Jambo muhimu zaidi duniani ni unga, tunakula, na sukari na mafuta. Tunatumai kuwa uamuzi huu utafutwa."